December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

REA: hatutawavumilia Wakandarasi wazembe,watoa rushwa

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) wameendelea kusisitiza utendaji kazi bora kwa wakandarasi wote nchini pindi wanapopata tenda za kupeleka umeme katika sehemu mbalimbali na kutokuwavumilia wakandarasi wazembe na wale ambao watajihusisha na uvunjifu wa maadili na uadilifu ikiwemo rushwa.

REA wametumia mkutano huo kutoa vyeti kwa baadhi ya wakandarasi ambao wamefanya vizuri kwa lengo la kuwaongezea nguvu, kuwatambua ili waweze kuhamasika zaidi kwa kufanya kazi kwa viwango vya ujenzi wa Tanesco, ubora wa vifaa, maadili na uadilifu na kuhakikisha wanajiepusha na rushwa.

Ameyasema hayo leo April 13, 2024 Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi, Hassan Saidy wakati wa mkatano na wakandarasi wa kujadili mradi mkubwa wa kupeleka umeme vijijini ifikapo mwezi 6 mwaka huu 2024.

“Lazima wakandarasi wafuate vigezo vya maadili ya Serikali na hatutawavumilia wakandarasi watakaojihusisha na rushwa, pia kuhakikisha wanawashirikisha viongozi wa Serikali ikiwemo Wakuu wa mkioa, wilaya na wabunge kupata taarifa kwa sababu hii ni miradi ambayo inafadhiliwa na serikali, hata kwa wenye viti wa vijiji ili waweze kunufaika” amesema Mhandisi Saidy

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tanesco kanda ya Mashariki Mhandisi Kenneth Boymanda ametumia nafasi hiyo kuwataka wakandarasi wote nchini kufanya kazi kwa spidi na viwango kwa sababu watanzania wanataka umeme hususani kwa wananchi wanaoishi vijijini tunaamini ukiendeleza vijiji taifa kwa ujumla uchumi utanyanyuka.

Aidha, Mhandisi Boymanda amewapongeza wakala wa nishati vijijini kwa kuwapa hamasa wakandarasi wanaofanya kazi vizuri katika ujenzi wa miundombinu ya umeme katika kuwafikishia wananchi waliyopo vijijini.

Naye, Mhandisi Shaban Zacharia kutoka kampuni ya STEG International Services amesema huwa kuna changamoto mbalimbali wanakutana nazo lakini wanaishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaunga mkono na kuhakikisha vikwazo hivyo vinakwamuliwa kwa wakati.