May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Pinda amshukuru Rais Samia ujenzi njia ya umeme

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MBUNGE wa Jimbo la Kavuu na Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Mhe. Geophrey Pinda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji mradi wa ujenzi wa njia ya umeme kutoka Inyonga hadi Majimoto katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.

Halmashauri ya Mpimbwe kwa sasa inapokea umeme kutoka Zambia ambao umeelezwa kukatika mara kwa mara kunakosababishwa na radi zinazopiga nguzo za umeme kwenye milima Lyambalyamfika inayotenganisha mkoa wa Rukwa na halmashauri ya Mpimbe.

“Mama tunakushukuru sana sisi wananchi wa Mpimbwe na Mlele. Pia nimshukuru Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Mpango alipotembelea kituo cha umeme Mlele alitoa maelekezo kuwa njia ya umeme kutoka Inyonga kwenda Majimoto ijengwe.

Nashukuru sana na huo ni ushahidi tosha kwamba sasa kazi imeanza utekelezaji” alisema Pinda.

Akizungumza wakati wa kukagua nguzo za
umeme kwa ajili ya utekelezaji mradi huo katika wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi tarehe 10 April 2024, Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema, uamuzi wa serikali kujenga njia ya umeme siyo tu utawasaidia wananchi na wafanyabiashara bali utachochea shughuli za maendeleo kwenye halmashauri ya Mpimbwe hususan wananchi wa jimbo lake la Kavuu.

Alibainisha kuwa, wananchi wa Mpimbwe
wamekuwa wakipata shida ya huduma ya
umeme alioueleza kuwa unakatika mara kwa mara na hivyo kuwafanya kushindwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

Aliwataka wananchi wa jimbo lake la Kavuu kuwa na subira wakati mradi huo ukitekelezwa huku akiwaeleza kuwa, mambo mazuri hayahitaji haraka na kusisitiza kuwa, mradi huo ni sehemu ya mafanikio makubwa ya jimbo na ni eneo ambalo serikali imelipa umuhimu wa pekee katika kusimamia na kuwaletea wananchi huduma mbalimbali kama vile umeme.

“Wafanyabiashara wenye mashine za kukoboa mpunga na mazao memgine ya
chakula wawe watulivu na baada ya miezi
michache ni kama opereshemi ya miezi miwili tutakuwa tuna umeme, utakapowashwa ule wa gridi ya taifa maana yake utawashwa mpaka jimbo la Kavuu ambalo kadhia ya umeme inaenda kumalizika” alisema.

Mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaji Majid Mjengwa alimueleza Mhe, Pinda kuwa, tayari wameanza kupokea nguzo kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa njia ya umeme kutoka Inyonga hadi Majimoto halmashauri ya Mpimbwe wenye urefu wa takriban kilomita 135 ambapo ameelezea hatua hiyo ni faraja kwao na wananchi wa Mlele kwa ujumla.

Mkuu huyo wa wilaya ya Mlele ameweka
wazi kuwa, wao kama wasimamizi wa mradi watahakikishia mahitaji yote muhimu kama vile ulinzi kwa watakaofanya kazi kipande chote cha hifadhi unaimarishwa.

“Mahitaji yote kama kuhakikisha askari wa
TAWA na wale wa wanyama pori wanakuwepo kutoa ulinzi kwa watakaofanya kazi kipande cha hifadhi, tutashirikiana nao kwa maana ya mkandarasi kuhakikisha hawakwami na tuko tayari kutoa usaidizi utakaohitajika” alisema Alhaji Mjemgwa.

“Tutahakikisha wanaofanya kazi hawakwami katika kipande chote cha hifadhi na sisi kama wasimamizi tutatoa usaidizi kutoka askari wa hifadhi pamoja na wale wa TAWA hawakwami” alisema Alhaji Mjengwa.

Mradi wa Ujenzi wa njia ya umeme wa Inyonga hadi Majimoto unaoenda sambamba na ule wa Gridi ya Taifa kutoka Tabora umeelezwa kuwa suluhusho la kukatika kwa umeme mara kwa mara na hivyo kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zao za kusindika mazao bila wasiwasi .