January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC.Senyamule:vijana tumieni maonesho ya miaka 60 ya JKT kujifunza jinsi ya kujiajiri

Na Zena Mohamed,TimesMajiraOnline,Dodoma.

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amewataka vijana wa mkoa huo kwenda kujifunza jinsi ya kujiajiri kwa kutumia mtaji kidogo na kupata kipato kikubwa katika maonesho ya miaka 60 ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) yanayoendelea mkoani hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana,kuhusu maonesho hayo Senyamule amesema kuwa maonesho hayo yanaendelea hadi Julai tisa katika viwanja vya SUMAJKT eneo la Medeli ambapo kazi zinazofanywa na Vijana wa JKT yani SUMAJKT,zinaoneshwa ikiwemo sekta ya Kilimo,mifugo,uvuvi,ujenzi,useremala na sekta nyingine.

“Na tunafahamu siku hizi wanataasisi inayojulikana kama SUMAJKT kama chombo au kama Kampuni ya biashara ndani ya JKT katika maonesho yale wanatoa elimu,ujuzi,maarifa na wanatoa mafunzo kwajili ya wananchi wanaotembelea maonesho yale muhimu,”amesema Senyamule.

Aidha amesema kuwa licha ya kuwepo kwa maonesho ya shughuli za sekta mbalimbali pia kuna zoo ya wanyama mbalimbali ambayo watu wanaweza kwenda kutalii.

“Kama mnavyojua Dodoma hatuna mbuga ya wanyama pori sasa wenzetu wa JKT watuletea wanyama pori ni fursa nzuri kwenda kutalii hapahapa Dodoma,”amesema Senyamule.

Maadhimisho hayo ya miaka 60 ya JKT yalizinduliwa Julai moja mwaka huu na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango nakutarajiwa kufikia kilele Julai 10 mwaka huu huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa mgeni akifunga maadhimisho hayo ya miaka 60 ya JKT.