May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ujenzi Bwawa la Yongoma kuanza

Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online

Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024 imepanga kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na ujenzi wa Bwawa la Yongoma lililopo Wilayani Same kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na kuinua kipato cha wakulima.

Hayo yamesema Julai 02, 2023 na Naibu Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde alipofanya ziara ya kikazi Wilayani Same kukagua maendeleo ya kilimo cha umwagiliaji na miundombinu yake katika kata za Ndungu,Miamba na Kihurio.

Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaendelea kukipa kilimo kipaumbele cha juu, ambapo bajeti ya mwaka 2023/2024 ametutengea fedha kiasi cha bilioni 970, kati ya fedha hizo zaidi ya bilioni 384 zimeelekezwa kwenye umwagiliaji”

Msukumo huo mkubwa kwenye kilimo unaooneshwa na Rais wetu mpendwa, ndo unapelekea Tume yetu ya Taifa ya Umwagiliaji kuendelea na ujenzi wa skimu, visima na mabwawa nchi nzima ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao nchini.

Tumesikia kilio cha wakulima wa Ndungu juu ya ukarabati wa skimu hii,katika bajeti ya mwaka 2023/24 tumetenga fedha za ukarabati na ujenzi wa Bwawa la Yongoma”alisisitiza Mavunde.

Awali, Wakitoa maelezo ya awali Mkuu wa Wilaya ya Same Kasilda Mgeni na Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki Anne Kilango-Malecela wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa namna inavyoendelea kuwakumbuka wananchi wa Same kwakuwa kupitia miradi hii ya umwagiliaji uzalishaji wa mazao utaongezeka na kukuza uchumi wa wananchi kwa kiwango kikibwa na kwamba kufuatia kazi hii nzuri ya serikali,wananchi hawatamsahau Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan na shukrani zao watazilipa mwaka 2025.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa alibainisha kuwa pamoja na upembuzi yakinifu, usanifu na ujenzi wa bwawa la Yongoma, Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2023/24 pia itafanya ukarabati wa mifereji ya skimu ya Ndungu ambayo inatoa maji mto Yongoma ili kuhakikisha wakulima wanufaika wapatao 3000 wanzalisha kwa tija kwenye hekta 680 za skimu hiyo,na itaendelea na ujenzi wa mifereji ya maji katika eneo la miamba na kusanifu bonde la mto saseni ili wananchi zaidi ya 68,000 wanufaike na kilimo cha umwagiliaji.