May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa awafunda watendaji sekta ya afya

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Ruvuma

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amewataka watumishi wa sekta ya afya mkoani hapa kuzingatia weledi na kutoa huduma bora kwa wananchi ili kuakisi maboresho na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta hiyo kupitia Bohari ya Dawa (MSD).

Kanali Ahmed amesisitiza kuwa, Serikali ya Rais Samia imetoa fedha nyingi kwa ajili ya maboresho na ujenzi wa miundombinu ya afya, hivyo ni lazima watendaji wafanye kazi kwa weledi mkubwa.

Kanali Ahmed ametoa rai hiyo hii jana wakati wa akifungua kikao kazi baina ya watendaji wa Bihari ya Dawa (MSD) Kanda ya Iringa na wadau wake kutoka halmashauri saba za Mkoa wa Ruvuma, ambazo ni Madaba TC, Madaba DC, Songea MC, Songea DC, Nyasa DC, Mbinga TC na Mbinga DC).

Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ruwiko, ulioko Manispaa ya Mji wa Songea.

Ametoa mfano uwekezaji uliofanywa na Rais Samia ambao ni pamoja na ujenzi wa majengo, ununuzi wa bidhaa za afya na kuwezesha ajira za kutosha, lengo likiwa kuinua hadhi ya huduma zinazotolewa nchini, hasa zinazomgusa Mtanzania wa kawaida.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwakumbusha viongozi hao wa sekta ya afya mkoani humo, kufanya maoteo yao ya bidhaa za afya kwa usahihi, umakini na kwa wakati ili kuiwezesha MSD kutekeleza majukumu yake ya ugavi wa bidhaa za afya kwa weledi.

Ahmed amewataka pia watendaji hao kusimamia ukusanyaji wa mapato, na kutumia vyema vyanzo vyao vingine vya mapato katika kulipa madeni ya MSD, huku akiwakumbusha pia kuhakiki taarifa sahihihi za utunzaji na utoaji wa bidhaa za afya, ili kuepuka upotevu wa bidhaa hizo.

Katika hatua nyigine, Mkuu huyo wa mkoa ameipongeza MSD kwa utendaji wake katika kuboresha hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya, huku akiwapongeza kwa kuitisha mkutano huo wa wadau kwani utasaidia kuboresha mahusiano na mawasiliano.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ugavi na uendeshaji wa MSD Victor Sungusia, amebainisha maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanywa na MSD katika nyanja mbalimbali kupitia majukumu yake makuu ya uzalishaji, ununuzi, utunzaji na usambazaji.

Sungusia alibainisha jinsi MSD ilivyojizatiti katika utekelezaji wa majukumu yake kupitia mifumo ya kisasa ya kidigitali, ugatuzi wa majukumu ya Kanda, ujenzi wa viwanda mbalimbali vya dawa na vifaa tiba, maboresho ya mfumo wa usambazaji wa bidhaa na mengine.