Na Crecensia Kapinga, TimesMajira,Online, Songea
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Generali Balozi Wilbert Ibuge, amewataka majaji, mahakimu na mawakilli mkoani hapa kutojihusisha na vitendo vya rushwa,ubaguzi,upendeleo ikiwemo uvunjifu wa sheria za nchi.
Badala yake amewataka watambue kuwa vitendo hivyo vinaharibu taswira nzuri ya mhimili huo na kwamba wanapaswa kujua kuwa Mahakama imepewa uwezo na haki za Kimungu.
Kauli hiyo imetolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Generali Balozi Ibuge kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini ambayo kimkoa yalifanyika kwenye Viwanja vya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea.
Amesema kuwa mahakimu na mawakilli wote katika Mkoa huo wanatakiwa kutoa huduma kwa wananchi hususani wa vijijini kwa wakati na kuzingatia sheria, kwani haipendezi kuona wananchi wakilalamika dhidi ya kutotendewa haki au kucheleweshwa kupatiwa haki.
Mkuu huyo wa Wilaya Mgema amesema wananchi hawana sababu ya kuamini wanayoamua, hivyo ni vyema wakamuomba Mungu ili matendo yao yasitiliwe shaka juu ya usahihi wa maamuzi wanayoyatoa.
Hata hivyo, amewapongeza kwa utendaji wao mzuri wa kazi kwa sababu hajawahi kupata malalamiko yeyote hivyo ni uhakika tosha kuamini wanafanya kazi vizuri.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Muu ya Tanzania Kanda ya Songea, Sekela Moshi amesema mahakama kama chombo kingine chochote kinachotoa huduma katika jamii ya zama za mapinduzi ya nne ya viwanda ambapo maendeleo na matumizi ya TEHAMA katika kuboresha mifumo yake ya utoaji haki ili kuendana na kasi ya maendeleo ya jamii ya zama za mapinduzi ya nne ya viwanda vinginevyo jamii itaiacha mahakama nyuma na itabaki na ombwe la chombo cha utoaji wa haki.
Aidha amewataka wananchi watambue kuwa wanawajibu wa kufuata taratibu za kisheria za mwenendo wa madai na kwa jinai kwa ngazi mbalimbali za mahakama kuliko kulalamika na kuitaka mahakama itende haki hata pale ambapo sheria hazikufuatwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Edson Mbogoro alisema Serikali ina jukumu la kuhakikisha inatenga bajeti ya kutosha kwa mahakama pamoja na taasisi zake zote zinazohusika na utoaji haki nchini itasaidia kuongezeka kwa majaji na mahakimu na hivyo kutasaidia kupungua ucheleweshaji wa mashauri mahakamani.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote