Na.Mwandishi Wetu,TimesMajira
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza mikakati thabiti ya kuboresha usafi wa mazingira, kuimarisha usalama na kukuza uchumi jijini humo, ikiwemo uzinduzi wa kampeni kabambe ya usafi itakayofanyika Novemba 14, 2026 katika viwanja vya Posta Kijitonyama chini ya kaulimbiu isemayo “Dar es Salaam Safi Inawezekana kwa Pamoja”.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Chalamila ameeleza kuwa jiji hilo huzalisha takribani tani 4,657 za taka kwa siku, hivyo kampeni hiyo itahusisha ugawaji wa vifaa vya usafi na pikipiki kwa ajili ya usimamizi mitaani, sambamba na kuingia makubaliano na mwekezaji kutoka Ghana atakayechakata taka hizo kuwa mbolea.
Kuhusu uendelezaji wa sekta isiyo rasmi na huduma za jamii, Chalamila amebainisha mipango ya ujenzi wa masoko ya kimkakati maeneo ya Tandika, Mbagala, pamoja na soko kubwa katika eneo la Kibungo/Sangisa litakalohudumia wafanyabiashara wadogo zaidi ya 14,000 ili kuwawezesha kufanya kazi katika maeneo rasmi kwa kuzingatia mipango miji.

Aidha, ameeleza kuwa mkoa unaandaa kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote, huku kukiwa na mikakati ya kuwasaidia wananchi wenye uhitaji kupitia wadau mbalimbali ili wapate huduma za matibabu bila vikwazo.
Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amekemea vikali vitendo vya ujambazi na uporaji vinavyohatarisha amani, akitolea mfano tukio la hivi karibuni la kuuawa kwa kijana mfanyabiashara aliyeshambuliwa na majambazi wenye silaha.

Amewataka wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu, akisisitiza kuwa Dar es Salaam ndiyo taswira na kitovu kikuu cha biashara na diplomasia nchini, hivyo usalama wa raia na mali zao hauwezi kufanyiwa mzaha.

More Stories
Magesa awataka watendaji kufuata sheria ukusanyaji wa mapato
Chalamila kwenda Qatar kuishangilia Serengeti Boys
Watanzania milioni 25 kunufaika na bima ya afya kwa wote