Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema anatarajia kwenda nchini Qatar kuishangilia timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) katika Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Novemba 19 hadi Desemba 13 mwaka huu.
Chalamila amesema mbali na yeye mwenyewe kwenda kuipa hamasa timu hiyo, pia kuna mpango wa kugharamia safari ya baadhi ya mashabiki wa Tanzania watakaopata fursa ya kwenda Qatar kushuhudia na kuishangilia Serengeti Boys.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Chalamila amewataka Watanzania kuungana na Serikali katika kuiunga mkono timu hiyo, akieleza kuwa kufuzu kwa Serengeti Boys kushiriki mashindano hayo ni hatua kubwa na ya kujivunia katika maendeleo ya soka la vijana nchini.
“ushiriki wa timu hiyo katika mashindano hayo makubwa duniani unapaswa kuwaunganisha Watanzania bila kujali tofauti zao, kwa kuwa Serengeti Boys inaiwakilisha nchi katika jukwaa la kimataifa.
Chalamila amesema mafanikio ya Serengeti Boys ni kielelezo cha matunda ya uwekezaji unaofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya michezo.
Aidha, ametoa wito kwa Watanzania kuwa wazalendo, kuungana na timu hiyo na kuipa sapoti ya kutosha ili iweze kufanya vizuri na kuipeperusha vyema bendera ya taifa katika mashindano hayo.
Amesisitiza kuwa hamasa kutoka kwa Watanzania ni sehemu muhimu ya kuijengea timu hiyo morali wakati ikijiandaa kukabiliana na wapinzani wake katika michuano hiyo ya kihistoria.

More Stories
Magesa awataka watendaji kufuata sheria ukusanyaji wa mapato
Rc.Chalamila atangaza rasmi mikakati ya kuboresha Dar
Watanzania milioni 25 kunufaika na bima ya afya kwa wote