Na Joyce Kasiki, Dodoma
WAZIRI wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema Serikali imelenga kuongeza idadi ya Watanzania wanaonufaika na Bima ya Afya kwa Wote kufikia milioni 25 ifikapo Juni 2027, kupitia awamu ya pili ya mpango huo iliyoanza Oktoba 22, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za matibabu bila vikwazo vya kifedha.
Amesema awamu hiyo inahusisha wananchi wenye uwezo wa kujilipia bima zao na familia zao kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) au kampuni binafsi zilizoidhinishwa, huku Serikali ikiendelea kugharamia bima kwa wananchi wasio na uwezo wa kujilipia.
Mchengerwa ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua semina maalumu ya kuwajengea uelewa Wabunge kuhusu utekelezaji wa mpango huo, ambapo amesema katika awamu ya kwanza kaya 201,376 kati ya 276,004 zilizotambuliwa kutokuwa na uwezo wa kujilipia bima zilihakikiwa na kupatiwa kadi, sawa na asilimia 73 ya lengo.
Aidha, amesema Mfuko wa Usawa unaogharamia bima kwa wananchi wasio na uwezo unatarajia kukusanya Shilingi bilioni 261.3 katika mwaka wa fedha 2026/2027, huku Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ukiwa umetambua kaya mpya 818,954 zinazostahili kusaidiwa.
Waziri huyo amewataka Wabunge kutumia nafasi zao kuwahamasisha wananchi kujiunga na mpango huo, huku akisisitiza umuhimu wa kuboresha huduma katika vituo vya afya, kuimarisha mifumo ya TEHAMA na kudhibiti udanganyifu ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dkt. Irene Isaka, amejibu hoja za Wabunge waliotaka kufahamu uwezekano wa kupunguziwa gharama za kifurushi cha bima hiyo ili kuwawezesha kusaidia wananchi wengi zaidi wenye uhitaji.
Hata hivyo, Dkt. Isaka amesema hakuna punguzo la gharama ya kifurushi hicho kwa sasa, akieleza kuwa kiwango kilichowekwa kinazingatia hali halisi ya utekelezaji wa mpango huo na mahitaji yake ya kifedha.
Amefafanua kuwa gharama ya bima hiyo ilipaswa kuwa Shilingi 350,000, lakini kutokana na watu wengi kusajiliwa kwa wakati mmoja, kiwango cha Shilingi 150,000 kimewekwa kuwa ndicho kinachotosheleza kwa utaratibu wa kifurushi hicho.

More Stories
Rc.Chalamila atangaza rasmi mikakati ya kuboresha Dar
Ujenzi wa njia ya umeme mafia,kuwanufaisha wakazi wa Mkuranga
Dc Shaka:Nendeni mkalinde nchi kwa wivu Mkubwa