May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Batilda ahamasisha kilimo cha Kakao

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

WAKULIMA Mkoani Tabora wameshauriwa kuanza kulima zao la kakao (cocoa) ili kupanua wigo wao katika mazao ya biashara na kunufaika na fursa ya masoko ya zao hilo iliyopo ndani na nje ya nchi. 

Ushauri huo umetolewa juzi na Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alipokuwa akiongea na Viongozi wa wakulima zaidi ya 450 kutoka vyama vya msingi (Amcos) zaidi ya 143 za Wilaya ya Urambo na Kaliua.

Alisema zao hilo ni miongoni mwa zao yenye bei nzuri katika soko la dunia kama ilivyo kwa mazao mengine wanayolima ya tumbaku na korosho na linaendana sana na mazingira ya Mkoa huo na haliathiri mazao ya msingi.

Alibainisha bei ya zao hilo kwa sasa kuwa ni sh 12,000 kwa kilo, tofauti na mazao mengine, hivyo kuwa kichocheo kwa wakulima wengi zaidi kulima, alitoa mfano wa wakulima wa Mkoa wa Mbeya wanaolima zao hilo kuwa wananufaika zaidi.

Katika kuonesha ari na hamasa yake kwa wakazi wa wilaya zote 7 za Mkoa, alisema tayari ameagiza miche 200 ya zao hilo ambayo italimwa kama mfano kwa wakulima wengine.

‘Nimeagiza miche 200 ili wananchi waone zao hilo linavyolimwa, ni zao rafiki kwa uoto na mazingira ya mkoa wetu pia ni zao rafiki kwa ufugaji nyuki, kilimo hiki kina tija kubwa kwa uchumi wa wananchi’, alisema.

Dkt Batilda alisema kutokana na Mkoa huo kuwa kitovu cha uzalishaji asali yenye ubora unaotakiwa katika soko la dunia, mazao mengine yote yatakayolimwa ni lazima yawe rafiki wa nyuki ili kuleta tija kubwa na yasiyo rafiki yaachwe.

Aidha alishauri Amcos zote kuhamasisha wanachama wao kukata bima ya mazao ili hata wakipata hasara kutokana na athari za tabia nchi waweze kupata fidia ya gharama ya mazao yao.

Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika Milambo Nteziliyo John alipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha shughuli za wakulima.

Alibainisha kuwa licha ya changamoto ndogondogo zilizopo, wanachama wao wameendelea kunufaika na mazao wanayolima ya tumbaku na korosho na kumhakikishia kuwa wapo tayari kupokea ushauri wowote unaolenga kumwinua mkulima kiuchumi.