April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RATCO: Wenye mji tumerudi kazini

Na Hadija Bagasha Tanga, TimesMajira Online

Halmashauri ya jiji la Tanga imesema haina ugomvi na msafirishaji yeyote ambaye atakuwa na kituo binafsi vya kukusanyia abiria (terminal) inayokidhi vigezo na kwamba wataendelea na msimamo wao wa kuzishughulikia teminal ambazo hazina sifa.

Meya wa jiji la Tanga Abdulrahman Shiloo ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa jiji la Tanga kwenye hafla ya uzinduzi wa huduma za usafirishaji za kampuni ya Ratco iliyopo jijini Tanga.

Kauli hiyo imekuja wakati ambao kukiwa na malalamiko kati ya wamiliki wa mabasi wenye vituo binafsi vya kukusanyia abiria vinavyokidhi vigezo na wale wanaoendesha vituo visivyokuwa na sifa ya kutolea huduma.

“Niwaambie wadau wa usafirishaji jijini Tanga kwamba sisi Halmashauri ya jiji la Tanga hatuna ugomvi na msafirishaji yeyote atakayeleta magari yake kwenye terminal inayokidhi vigezo ukiwa na terminal inayokidhi vigezo lete magari yako,”

Aliongeza kuwa terminal tunayoizungumza inatakiwa kuzingatia kuwa na sehemu ambayo mtu akihitaji kufanya ibada iwepo, kupata chakula, huduma za choo kwa jinsia zote lakini pia isiwe sehemu inayozuia barabara watumiaji wengine wakashindwa kupita.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa amesema watanzania walio wengi wana tabia ya kutokufanya kazi kwa bidii pindi wapatapo kazi jambo ambalo limekuwa likiibua mgogoro kati yao na waajiri.

Mgandilwa aliwataka wakazi wa Tanga kujituma pindi wapatapo kazi na badala yake waondoe visingizio vinavyoweza kusababisha kushindwa kufanya kazi kwa weledi ili waweze kujikwamua kiuchumi.

“Kuna changamoto ambayo nimekuwa nikikutana nayo ofisini kwangu mara kwa mara watu wanakuja kulalamika kuwa wameachishwa kazi au wameacha kazi sababu ya msingi Watanzania tulio wengi tunapokwenda kutafuta kazi mikono inakuwa nyuma lakini tukishapata kazi tunakuwa wa jeuri na mwisho wa siku tunashindwa kutimiza wajibu, “amesisitiza Mgandilwa.

Ameongeza kuwa mimi ndio Mkuu wa wilaya ya Tanga ninawajua wanatanga nawaombeni tusitie aibu za mtindo huu haipendezi asubuhi unatakiwa kwenda na gari unaanza visingizio tumbo linauma hivyo huwezi kwenda hicho kitu ninaomba tuache.

Aidha aliwasisitiza wanyakazi Katika kampuni hiyo ya Ratco Kutumia vyombo hivyo bila kuviharibu ili kufanya mapinduzi ya uwekezaji yenye manufaa kwa maslahi ya Mkoa na taifa kwa ujumla.

Naye mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Ratco Salim mohamed Ratco alisema kashawishika kuwekeza mkoani hapa kwa kuanzisha ruti za usafiri za mikoani ili kuleta mapinduzi ya uwekezaji wa usafirishaji na kwamba kilichowakwamisha hapo mwanzo ni tatizo la ugonjwa wa Uviko 19 na hivyo biashara kuwa ngumu.

Salim alisema katika kampuni yake atahakikisha anatoa huduma ya kisasa inayokidhi vigezo lengo likiwa ni kufanya mazingira ya abiria wawapo safarini kuwa rafiki nayo.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Tanga Adam Malima aliwataka wasafirishaji kuhakikisha wanafanya huduma yenye tija ili kuingia katika soko la ushindani wenye tija kwa masilahi ya umma.

Katika hafla hiyo madereva wametakiwa kuheshimu sheria za usalama barabarani baada ya kuonekana kuwa wengi wao wamekuwa ni chanzo cha ajali ambazo nyingi zimekuwa zikigharimu maisha ya watu.