May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia avunja rekodi ya miaka 11 vita dawa za kulevya nchini

Na Joyce Kasiki, TimesmajiraOline, Dodoma

SERIKALI chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imevunja ya miaka 11 kwa kukamata kilogramu milioni 1.965 kwa kipini Januari hadi Desemba 2023.

Kiasi hicho ni kikubwa ikilinganishwa na kilogramu 660,465 zilizokamatwa katika kipindi cha miaka 11 iliyopita.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Bunge na Uratibu, Jesta Mhagama, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Aidha, Waziri Mhagama, alisema watuhumiwa 10.522 wamekamatwa katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2023 kati yao wanaume ni 9,701 na wanawake ni 821.

Ameongeza kwamba jumla ya hekari 2,924 za mashamba ya bangi na mirungi ziliteketezwa. “Hiki ni kiasi kikubwa sana cha dawa za kulevya kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja pekee, kwani kinazidi kiasi cha kilogramu 660,465 zilizokamatwa katika kipindi cha miaka 11.”

Waziri Mhagama ameongeza kwamba; “Serikali imefanikiwa kuzuia uingizaji wa kilogramu 157,738.55 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya kinyume cha sheria.”

Kwa mujibu wa Mhagama ili kuhakikisha jamii inapata uelewa juu ya tatizo la dawa za kulevya, Serikali imepanua wigo wa utoaji elimu kwa kuelekeza nguvu kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo.

Amesema kupitia taasisi hizo Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanania (TAKUKURU) ili kutoa elimu ya dawa za kulevya na rushwa kupitia klabu za kupinga rushwa nchini, ambapo sasa zitaitwa klabu za kupinga rushwa na dawa za kulevya.

“Tafiti zinaonesha kwamba, matumizi ya dawa yanaanza katika umri mdogo kati ya miaka 10 na 12, hivyo Serikali imeona iweke mkazo huko, kwani watoto wengi wanapitia katika shule hizo,“amesema

Pia amesema, elimu imeendelea kutolewa kwenye makundi mbalimbali ya kijamii yakiwemo ya viongozi wa dini, viongozi wa kimila, waandishi wa habari, vyombo vya ulinzi na usalama, maofisa forodha na wakulima hasa katika maeneo yaliyokithiri kwa kilimo cha bangi na mirungi.

Kwa upande wa tiba, amesema Serikali imeendelea kuimarisha huduma kwa kuongeza vituo vya kutolea tiba kwa waraibu kwa kutumia dawa na huduma za unasihi (MAT) ambapo kwa mwaka 2023 kituo kimoja kimefunguliwa mkoani Morogoro katika Gereza la Kihonda, ambapo hadi kufikia Desemba 2023, jumla ya vituo 16 vilikuwa vinatoa huduma kwa walengwa.

Aidha, vituo vingine viwili katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga na Chalinze mkoani Pwani vinatarajia kukamilika ifikapo Aprili mwaka huu.

Aidha, amesema Serikali iko kwenye hatua za mwisho za ujenzi wa kituo kikubwa cha huduma za Tiba na utengamao katika jiji la Dodoma, ambacho mbali na huduma za matibabu pia yatatolewa mafunzo maalumu yatakayowawezesha waraibu kujitegemea kimaisha baada ya kukamilisha safari ya matibabu yao.

Vilevile amesema,Serikali imekamilisha ujenzi wa maabara ya kisasa itakayotumika kwenye utambuzi wa sampuli mbalimbali za dawa za kulevya pamoja watu wanaotuhumiwa kutumia dawa hizo.