May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia aungwa mkono na wanafunzi wasioona

Na Lubango Mleka, TimesMajira Online

Mabadiliko ya tabianchi ni ongezeko la muda mrefu la joto la wastani la dunia ambalo husababisha kubadilika kwa mfumo mzima wa hali ya hewa.

Ambao mara nyingi matokeo yake huleta athari hasi katika jamii kama vile ukame, mafuriko, kuongezeka kwa hewa ukaa, kwani kwa maeneo oevu na kuanguka kwa theluji.

Mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazoukabili  Mkoa wa Tabora, Tanzania na dunia kwa ujumla.

Hiyo katika kukabiliana na changamoto hiyo na  kuunga juhudi za Rais Dkt Samia Hassan Suluhu, NEMC na wizara ya Mazingira, Taasisi ya Akili Platform Tanzania imeamua kupanda miche katika shule ya watoto wasioona ya Furaha iliyopo Manispaaa ya Tabora mkoani Tabora kwa kupanda miche zaidi ya 100 ya Matunda.

Hivyo kupungua kwa misitu kunakosababishwa na uvunaji wa miti,ongezeko la shughuli za viwanda duniani, kupungua kwa theluji, mabadiliko ya utaratibu wa mvua , mafuriko na ukame miongoni mwa jamii nyingi ulimwenguni zimekuwa zikisababisha athari hasi za mabadiliko ya tabianchi.

Ili jamii yetu ijinusuru kutoka kwenye changamoto hizo zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi wataalamu wa mazingira kutoka NEMC wanashauri kuwa njia mojawapo ni kupanda miti kwa wingi katika jamii zetu ili kuokoa maisha ya viumbe hai wengine pamoja na binadamu.

Pamoja na kuwa na faida zake nyingi kama vile kulinda vyanzo vya maji, kuvuta mvua, kuwa makazi ya viumbe hai mbalimbali, kutoa nishati ya kuni, mkaa na kutoa mbao, miti pia husaidia kunyonya na kuhifadhi hewa ukaa inayozalishwa na binadamu kutokana na shughuli zake mbalimbali.

Madhara yatokanayo na hewa ukaa ni pamoja na kutoboka kwa tabaka la ozoni na kusababisha miale mikali ya jua kuufikia uso wa dunia hali inayosababisha ongezeko la joto na kukauka kwa mimea, ukame na hata maradhi kwa viumbe hai wengine pamoja na binadamu, hivyo jamii isipojenga tabia ya kupanda miti itasababisha kupotea kwa viumbe hai wote.

Hata hivyo vyanzo vingi vya maji huanzia kwenye sehemu zenye miti mingi (misitu) juu ya milima ambapo huanza kama chemchem kisha vijito halafu maji hutiririka kama mto.

Kazi ya miti ni kuzuia maji kuzama ardhini (mizizi) na pia majani ya miti huzuia maji maji yasichukuliwe kama mvuke.

Upandaji miti na uhifadhi wa misitu ni moja ya hatua muhimu sana katika kukabiliana na tatizo la ukame katika nchi nyingi Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania.

Tayari nchi kupitia taasisi inayosimamia mazingira imeanza mikakati madhubuti ya kupanda miti nchi nzima kuanzia shuleni chini ya kampeni isemayo “SOMA NA MTI” ambayo tayari imeishazinduliwa na Waziri mwenye dhamana ya kusimamia Mazingira Dkt. Seleman Jafo.

“Upandaji na uwepo wa misitu katika jamii zetu unachangia asilimia 47 ya akiba ya hewa ukaa ya misitu duniani na hutoa asilimia 60 ya miti ya mbao inayotumiwa viwandani duniani, ambayo inaweza kutumika kuzalisha mazao endelevu ya misitu ili kusaidia mchakato wa kimataifa wa kuingia katika uchumi unaojali mazingira, kudumisha uwiano kati ya uhifadhi na uzalishaji katika mabadiliko ya tabianchi kunahitaji mfumo wa sera kamilifu na endelevu,”.

Ambapo  NEMC, Wizara ya Mazingira, Taasisi ya Akili Platform Tanzania imedhimisha miti  kwa kupanda miche ya miti ya matunda zaidi ya 100, katika shule ya watoto wasioona ya Furaha iliyopo Manispaaa ya Tabora mkoani Tabora, ikiwa ni moja ya jitihada za kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi na kuunga mkoani juhudi za Rais Samia katika kulinda na kutunza mazingira.

Mkurugenzi wa taasisi ya Akili Platform Tanzania na Balozi wa Mazingira,Roghat Robert, anasema kuwa  Tanzania kama taifa linahifadhi na kuthamini mazingira ya asili kwa njia mbalimbali kulingana na miongozo ya kitaifa na kimataifa.

 Kwa sababu hiyo, ni jukumu la wote  kuhakikisha kuwa wanakuwa na mkakati wa uhifadhi wa kudumu wa rasilimali hizo zinazotunza mazingira yetu.

Anaeleza kuwa wamechagua shule ya msingi Furaha kama kituo cha maadhimisho ya siku hiyo kitaifa ikiwa ni  kuonesha upendo hata kwa wale walio na ulemavu kwani kupanda miti ni hatua muhimu katika kuhifadhi mazingira  kwa vizazi vijavyo.

” Ninayo furaha kubwa kuwepo hapa leo kusherehekea siku ya kupanda miti katika shule ya msingi Furaha shule pendwa sana yenye wanafunzi wasiona kama kitovu cha Akili Platform Tanzania kitaifa cha siku ya leo,”anaeleza Robert na kuongeza kuwa 

“Hii ni siku muhimu sana kwa sisi sote kwani inatuwakilisha wajibu mkubwa tunao sisi kama Akili platform Tanzania hususani Idara ya Mazingira katika kusimamia mazingira yetu, kuongeza na  kukuza utamaduni wa kupanda miti katika jamii zetu kwa kushirikiana na mabalozi wa mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na wadau mbalimbali.”

Pia anaeleza kuwa miti ni kichocheo muhimu katika kusimamia ubora wa hewa, kupunguza hali ya joto na mafuriko,kukuza uchumi wa nchi yetu, kutupatia matunda, kupata dawa na fursa nyingine.

Kama wanataka kuendelea kutumia rasilimali hiyo muhimu,wanahitaji kuwa na mkakati madhubuti wa kupanda miti zaidi, na kuhakikisha kuwa wingi wa miti inahimili mabadiliko ya hali ya hewa.

Kwa kuzingatia hilo Akili platform Tanzania imekuja na mpango mkakati wa kuanzisha kitalu cha miti ambacho kipo katika hatua za awali za kukamilishwa kwa Mkoa wa Tabora Wilaya ya Tabora Mjini Kata ya Cheyo na badae itakuwa kila sehemu iliyo na ofisi ya Akili Platform Tanzania. 

Aidha, anaeleza kuwa  Akili Platform Tanzania kuanzia mwezi Januari mpaka kufikia Aprili mwaka huu  imeisha panda miti zaidi ya  5000, kupitia kampeni yake ijulikanayo ‘GO GREEN BE FREE FROM MENTAL CHALLENGES CAMPAIGN 2023-2024’, pia zoezi la kuikagua linaendelea na linatia matumaini makubwa sana.

Hiyo yote ni kuonesha utendaji kwa vitendo na si kwa maneno tu, ambapo Aprili 22,2023 jumla ya miti 1500  imepadwa chini ya Akili  Platform Tanzania kwa baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja na shuleni,nyumbani na vyuoni.

“Kupanda miti sio suala la sheria ya  mtu binafsi, ni suala linalohusu jamii nzima,ni wajibu wetu kila mmoja kuhakikisha  tunachangia kikamilifu katika kampeni hii ya kupanda miti, kwa sababu ni uzito wa wote kuilinda, kuitunza, na kuwaacha vizazi vijavyo waweze kufurahia fursa kubwa za mazingira ambazo tunazo sasa,”anaeleza Robert.

Vilevile anaeleza kuwa kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya mazingira na afya ya akili kwani mabadiliko ya hali ya hewa na uharibifu wa mazingira hupelekea ugonjwa wa kiwewe kutokana na kumbukumbu za majanga mtu aliyo yapitia kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa mfano mafuriko.

Kadhalika mazingira asilia yana uhusiano uliopo kati ya afya ya akili na mazingira asilia ni kwamba  hupunguza mawazo, kuboresha hisia na  kuboresha ustawi wa afya ya akili.       

“Na2tumaini kuwa leo na siku za usoni, tutakuwa tayari kupanda miti kwa wingi, kwa sababu yote yamefanyika katika kuiweka Tanzania kama nchi iliyojitolea kikamilifu katika kufanya kila jambo linalowekwa mbele yetu siku za kesho kwa utunzaji wa vizazi vijavyo, kauli mbiu yetu ni  Tazama,Tafakari,Tenda kwa busara tunza afya ya akili na Mazingira ulipo,”. 

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Furaha Ibrahim Suleiman na Mwalimu wa mazingira Rehema Shimba wameipongeza taasisi ya Akili kwa kuwakumbuka na kushiriki nao katika siku hii muhimu ya upandaji miti Duniani.

“Kwanza kabisa niipongeze taasisi hii kwa kutuona na kuja kushiriki nasi katika siku hii muhimu ya upandaji miti, kwani wametupatia miche 100 ya matunda hivyo itakapokuwa wanafunzi wetu watapata matunda na kuboresha afya zao,”anaeleza Selemani.

Anaeleza kuwa mbali na faida za miti, kupitia  siku hiyo mazingira ya shule hiyo yatazidi kuwa bora na kuongeza mvuto kwa wananchi na kuwa mfano katika kutunza mazingira, hivyo waliahidi kuunga mkono juhudi za Rais  Samia katika kutunza  mazingira.

Nao baadhi ya  wanafunzi wa shule hiyo  Shija Makoye na Kusekwa Lazaro, wameshukuru kwa kukumbukwa na taasisi ya Akili Platform katika kuunga juhudi za upandaji miti na utunzaji mazingira.

“Nimefurahi sana kupanda mti leo na ninaahidi kuutunza ili kutunza mazingira  na kulinda mabadiliko ya tabia nchi, hivyo naomba na taasisi zingine ziunge mkono juhudi hizi isiishie hapa tu ipandwe miti katika shule zingine za watoto wenye uhitaji maalumu kama sisi,”anasema Lazaro.