May 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia atoa zawadi kwa wajukuu wake

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa zawadi maalumu kwa wajukuu wake wanaolelewa katika Kituo cha Mafanikio Foundation kilichopo Kata ya Bachu Mjini Tabora.

Zawadi hiyo imekabidhiwa Machi 4,2024 na Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),Aziza Sleyum katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Cha Utumishi wa Umma (TPSC) mjini hapa.

Amesema kuwa zawadi hiyo ya mashine ya kudurufu karatasi (printer) ni msaada muhimu sana kwa kituo hicho kwa kuwa itawarahisishia utendaji viongozi na Walimu wa taasisi hiyo ikiwemo utoaji elimu ya dini ya Kiislamu kwa watoto hao.

Amefafanua kuwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho ni yatima na wengine walikuwa wanaishi katika mazingira magumu, hivyo ametoa pongezi kwa viongozi ambao wanawapa malezi mazuri.

‘Watoto hamjambo?, Bibi anawasilimia sana, amewaletea zawadi nzuri, pokeeni zawadi mliokuwa mnahitaji kwa muda mrefu, naamini itawasaidia katika shughuli zenu za kila siku, naomba muitunze na muitumia vizuri,”amesema.

Mbunge huyo ameeleza kuwa watoto wakilelewa katika mazingira mazuri na kupewa elimu ya dini watakua vizuri na kuwa na maadili mema, hivyo akatoa wito kwa wazazi na walezi kulea watoto wao vizuri ili wasiwe na tabia mbaya.

Amesisitiza kuwa mtoto akikosa malezi mazuri katika umri mdogo ataharibika mapema na akikua itakuwa vigumu sana kumbadilisha, hivyo akaomba wazazi, walezi na walimu kuwaangalia kwa umakini mkubwa watoto ili wakue vizuri.

Mkurugenzi wa Kituo hicho Amir Hussein Mikombe amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia zawadi hiyo wajukuu zake na kubainisha kuwa itakuwa kichocheo kikubwa cha kutoa huduma bora kwa watoto hao.

Ameongeza kuwa mbali na kupokea zawadi hiyo kutoka kwa Rais pia wametumia hafla hiyo kuzindua sera ya uhifadhi wa Quran Tukufu kwa watoto hao ili kuwaongezea ufahamu wa maandiko matakatifu ya dini ya Kiislamu.

Baada ya kupokea zawadi, wajukuu hao walifanya dua maalumu ya kumwombea Bibi yao Rais Samia ili Mwenyezi Mungu aendelee kumuongoza vizuri zaidi katika utendaji wake na wasaidizi wake na siku nyingine awaletee zawadi tena.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tabora Mjini Chifu Silvester Yared alipongeza kazi nzuri inayofanywa na Taasisi hiyo kwa kuwapa malezi ya kiroho na kimwili, aliongeza kuwa malezi mazuri kwa watoto hujenga jamii bora.

Akitoa salamu katika hafla hiyo Shehe Mahafudh Anan ameitaka jamii kuthamini elimu ya dini na kuwataka waumini wa dini hiyo kupeleka watoto wao madrasa ili wapate elimu mapema na sio kuita walimu nyumbani kuja kufundisha watoto wao.

Katika hafla hiyo mashehe na wageni waalikwa walifanya dua maalumu ya kumwombea Rais Samia, Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Mzee Hassan Wakasuvi.