May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia atoa maelekezo muhimu sita matumizi ya nishati safi ya kupikia

Asema Agosti ni mwisho wa taasisi zinazohudumia watu 100 kutumia kuni, mkaa, asisitiza matumizi nishati safi ya kupikia sasa lazima

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

RAIS Samia Suluhu Hassani, amezindua Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia huku akitoa maagizo sita, likiwemo la kumtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuandaa katazo kwa taasisi zote zinazohudumia watu kuanzia 100 kutotumia kumkaa na kuni kupikia.

Rais Samia amesisitiza kuwa baada ya miezi mitatu kutoka sasa ifikapo Agosti, mwaka huu kusiwe na taasisi inayohudumia watu kuanzia 100 inayotumia mkaa na kuni.

Rais Samia ametoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Maagizo mengine aliyotoa Rais Samia ni kuitaka Wizara ya Nishati ihakikishe inawafikishia mkakati huo wadau wote muhimu kwa manufaa ya wananchi na wadau kwa ujumla. Pia ametaka mkakati huo utafsiriwe kwa kiswahili na kingereza.

Aidha, Rais Samia ameitaka Wizara ya Nishati ikae na wadau wanaohusika serikalini na sekta binafsi kubaini maeneo ambayo yakifanyiwa kazi yatasaidia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa gharama himilivu.

Tatu, Rais Samia ameitaka wizara hiyo ishirikiane na wadau kuhakikisha wanakuwa na mfuko wa kuendeleza nshati safi ya kupikia ifikapo 2025. Aliitaka wizara na wadau waje na sheria itakayoanzisha mfuko huo na watajua namna ya kutafuta fedha ya kuendeleza mfuko huo.

Nne, Rais Samia ameitaka Ofisi ya Rais TAMISEMI iboreshe mikataba wanayoingia na wakuu wa wilaya ilikuongeza kifungu cha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kipengele cha kupima utendaji kazi wao.

Pia amesema ni vizuri TAMISEMI iwatambua wadau wanaotekeleza miradi ya nishati safi ya kupikia ili mafanikio yanayopatikana yaweze kupelekwa maeneo mengine. Alitaka sekta binafsi ifunguliwe njia.

Agizo la tano, ameitaka REA kujipanga vizuri kutekeleza majukumu yao yaliyomo kwenye Mkakati wa Taifa wa Matumizi wa Nishati Safi ya Kupikia.

Sita, amesema miezi mitatu ijayo ifikapo Agosti, Waziri Majaliwa aandae taarifa ya utekelezaji, kwani walisema taasisi zote zenye kuhudumia watu zaidi ya 100 zisitumie mkaa na kuni.

Amemuagiza Waziri Mkuu kuandaa katazo la kupiga marufuku taasisi zote zinazohudumia zaidi ya watu 100 kutumia kuni na mkaa. Alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia ni ya lazima na sio anasa tena.

Aidha, ameagiza Wizara ya Nishati kuongoza Watanzania kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa wananchi kwa bei inayohimilika.

Aidha, amesema wanatarajia sekta binafsi kuongeza uwekezaji pamoja na upatikanaji wa nishati safi ya kupikia sehemu mbalimbali nchini, lakini pia walete teknolojia rahisi inayowezesha wananchi kupata nishati safi kadri ya uwezo wao.

“Kwa mfano kulipia kadri anavyotumia kama inavyofanyika kwa umeme au maji,” amesema Rais. Amesema moja kati ya maonesho ya mazingira aliyoshiriki aliona wametengeneza mtungi ambao mtu analipa jinsi anavyolipia.

“Kuna mitungi inajazwa mtu kama ana 10,000 anatumia gesi ya elfu 10, ikimalizika mtungi unakata hata kama gesi ipo mpaka ulipe waje wakufungulie utumie tena,” amesema Rais Samia.

Ametaka watu hao watafutwe au wajitokeze ili wafanye nao kazi katika eneo hilo. Aidha, aliagiza kuvutia uwekezaji kwenye uzalishaji wa majiko banifu na sanifu ya umeme na kuhamasisha uzalishaji wa vifaa na mitungi ya gesi asilia hapa hapa nchini.

Amesema hatua hizo zitakuza uwekezaji na ajira kwa vijana na zitasaidia kupunguza gharama za nishati. Alisema yapo masuala yanawataka Serikali na sekta binafsi kukaa pamoja ya kuongeza ubunifu katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazochangia matumizi madogo ya nishati hiyo.

Rais Samia amesena waangalia namna wanavyoweza kuendeleza kuongeza matumizi ya nishati ya umeme kwa ajili ya kupikia. Aliwataka watu wabadilike.

Aidha, amesema sekta binafsi wana kazi ya kufanya kwa kuwezesha wadau wa sanaa kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati ya kupikia.

Ili kufanikiwa hilo, amesema wanahitaji ushirikiano wa wadau wote. Alihimiza sekta binafsi ijengewe mazingira ya kwenda hadi vijijini kwenda kupeleka vituo vya kujazia mitungi.