May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Samia mgeni rasmi maadhimishi miaka 85 ya TAG

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya miaka 85 ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God(TAG) ambayo yatafanyika Julai 14, mwaka huu katika viwanja vya uhuru Jijini Dar es salaam.

Hayo yamebainishwa Jijini Dar es Salaam jana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Mchungaji Dkt. Barnabas Mtokambali wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kilele cha maadhimisho hayo.

Amesema dhima ya maadhimisho hayo ni kumshukuru Mungu kwa uaminifu wake na kuliwezesha kanisa hilo kubaki imara kama Taasisi kwa miaka 85.

Mchungaji Dkt. Mtokambali amesema kuelekea maadhimisho hayo wamejikita katika maeneo matatu ya kumshukuru Mungu ikiwa ni pamoja na agizo kuu, kuzaa na kulea viongozi pamoja na miradi ya maendeleo.

“Kilele cha Maadhimisho haya ni fursa adhimu ya kuungana pamoja na waumini, viongozi wa dini, viongozi wa Serikali kumshukuru Mungu na kumtukuza kwa ajili ya miaka 85″alisema Dkt Mchungaji Mtokambali na kuongeza;

“Tunataka kuweka historia mpya ..tunataka kudhibitisha dhamira yetu ya kuendelea kuwa chanzo cha matumani, amani , upendo na mabadiliko chanya katika jamii, “amesema Mchungaji Dkt Mtokambali

Aidha amesema Kanisa hilo linajivunia kuwa sehemu ya Tanzania na kuhakikisha wanaendelea kuchagia katika maendeleo ya nchi .

Pia amesema wamekusudia kufanya ibada kubwa ya kumshukuru Mungu ambapo shughuli mbalimbali zimeandaliwa zinazolenga kuwahamasisha watu kutimiza Umoja na mshikamano na kujenga mazingira ya furaha na shangwe.

“Kupitia kilele cha maadhimisho haya tutafanya makongamano ya vijana zaidi ya elfu 10,000 wenye umri wa chini ya miaka 34 nchini kote, pamoja na semina maalumu ya uongozi kwa viongozi wa ngazi za juu wa Serikali Jeshi na Polisi pamoja na mikutano mikubwa ya injili.”amesema Mchungaji Mtokambali

Pia amesema kutakuwa na semina maalumu ya viongozi wa ngazi za juu wa dini na madhehebu mbalimbali, pamoja na kutoa huduma za kijamii, ikiwemo kuwafikia watoto takribani elfu 6000 wa Shule za Msingi za Jiji la Dar es salaam sambamba na kutoa taulo za kike kwa wasichana.

Vilevile amesema wameandaa shughuli za kuchangia katika miradi ya maendeleo ya jamii kama uchimbaji visima vya maji safi katika shule za msingi Jijini Dar sa salaam .

“Katika mradi wa uchimbaji wa visima vya maji tunaunga mkono jitihada za Rais Dkt Samia za kumtua mama ndio kichwani kwa kumuondolea mtoto kero za maji kichwani,”amesema Mchungaji Dkt Mtokambali.