Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar
RAIS Samia Suluhu Hassan, ameahidi ifikapo mwaka 2030 asilimia 88 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Aidha, ameahidi kuendelea kuwawezesha Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ili ifikapo mwaka 2030 zaidi ya asilimia 88 wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Ahadi yangu kwenu ni kuhakikisha asilimia kubwa ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia na hili nitalivalia njuga, kuhusu masuala ya jinsia na watu wenye makundi maalum nitaendelea kusimamia kuhakikisha tunaondokana na changamoto zilizopo.”
Ameyasema hayo juzi alipozungumza kwa njia ya simu na wanawake waliojitokeza katika kongamano la kumpongeza kwa kuwa kinara wa nishati safi ya kupikia, mazingira na afya ya mama na mtoto yaliyofanyika katika Ukimbu wa Diamond Jubelee Dar es Salaam, ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kumuunga mkono, Rais Dkt. Samia ili aweze kutimiza maono yake ya kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, utunzaji wa mazingira pamoja na uimarishaji wa afya ya mama na mtoto kwa tija na ufanisi mkubwa.
Aidha, amewataka watendaji wote wanaosimamia miradi ya nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira wahakikishe wananchi wote wanashirikishwa kikamilifu katika kampeni zote ili nchi ipate matokeo ya haraka.
“Taasisi zinazohusika na masuala ya nishati ziimarishe kampeni za kuonesha madhara ya nishati ngumu na mifumo ya upatikanaji wa nishati safi ili wanajamii wengi wahamasike katika kuingia kwenye mabadiliko ya nishati safi.”
Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa vyombo vya habari na wasanii kushirikiana na Serikali katika kubeba ajenda ya matumizi ya nishati safi ili kuongeza uelewa katika jamii na kuepuka magonjwa ya mfumo wa hewa, macho na kupata muda wa kutosha wa kufuatilia malezi kwa kuokoa muda unaotumika kutafuta nishati ngumu.
“Wizara zisimamie kikamilifu taasisi za umma na binafsi zilizo chini yao ambazo zinazotoa huduma kwa watu wengi kwa siku (100 hadi 300) ili zisitishe matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia katika nishati safi”.
Kwa upande, wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo, amesema Rais Dkt. Samia anastahili kuitwa “Championi” wa nishati safi ya kupikia na mazingira kutokana na jitihada kubwa alizozifanya kwa kutengeneza fursa za Watanzania kutumia nishati hiyo ikiwa ni pamoja na kusisitiza masuala ya utunzaji wa Mazingira.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amewataka wanawake kushirikina bega kwa bega kumlinda Rais Dkt. Samia kutokana na jitihada zake na mageuzi makubwa aliyoyafanya ambayo yanamgusa mwanamke na jamii kwa ujumla hususan katika uboreshaji wa miundombinu ya afya, maji na nishati.
Naye, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Doroth Gwajima amesema Rais Dkt. Samia ameendelea kuonesha uongozi unaojali masuala ya jinsia na makundi maalum, kwa kuanzisha Wizara Maalum pia kuwekeza katika miundombinu ya elimu kwa watoto wakike sambamba na kuwezesha mifumo rafiki kwa wanawake.
Awali, akizungumza katika Mkutano huo Mwenyekiti wa Balaza la Uwezeshji Wananchi Kiuchumi, Beng Issah amesema siku hiyo ni maalum kwa ajili ya kuweka alama ya kutambua jitihada kubwa zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha maisha ya watanzania.
Katika mkutano huo, Majaliwa aliendesha harambee ambayo ilifanikisha kupatikana kwa sh. Milioni 120 kwa ajili ya kumuwezesha Rais Dkt. Samia, kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Urais katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa