January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia amjulia hali mama mzazi wa Halima Mdee

 Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtembelea na kumjulia hali mama mzazi wa mbunge wa viti maalumu, Halima Mdee, Theresia Mdee, aliyelazwa katika Hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma.

Rais Samia amefika hospitalini hapo akiwa ameambata na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na viongozi wengine. Mara baada ya kufika alipokelewa na Mdee pamoja na mbunge mwenzake, Esther Bulaya.

Furaha imeongezeka zaidi pale mama yake na Mbunge huyo (Theresia Mdee) alipoeleza mapenzi yake kwa Rais Samia.

Mara baada ya kauli hiyo, Mdee alimwambia Rais Samia kwamba mara kadhaa mama yake amekuwa akimuuliza kuhusu harakati zake za kisiasa zenye mrengo wa kuisumbua Serikali inayoongozwa na Rais Samia.

“Yaani anakupenda kweli hadi wakati mwingine tukiwa wakali kidogo, ananiambia sasa nyie mnamsumbua mama yenu, namwambia tuache tu tuko kazini,” amesema Halima.  

Majibu hayo yalionekana kumkuna Rais Samia ambaye aliangua kicheko akisema; “Kumbe nina watetezi, hiyo ndiyo bahati yangu wanawake hawana compromise.”  

Aidha, Rais Samia alipata fursa ya kupiga picha na wauguzi na wakati akiondoka alisema, “Endeleeni kuchapa kazi, kumrudishia mtu uzima wake mna fungu kubwa kwa Mungu, hivyo nawaomba msichoke. Mie najituma sichoki, hivyo nawaomba na nyie msichoke.”