Na Bwanku M Bwanku,Timesmajiraonline,Dar
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan yuko ziara nchini Uturuki kuitikia mwaliko wa Rais Recep Tayyip Erdogan wa nchi hiyo.
Katika ziara hiyo Rais Samia pamoja na mazungumzo na Mwenyeji wake Rais Erdoghan, anatembelea maeneo yenye fursa mbalimbali pamoja na kuwashawishi wafanyabiashara wakubwa wa Uturuki kuja kuwekeza Tanzania katika sekta za Elimu, afya, kilimo na viwanda.
Uturuki ni moja ya mataifa 20 tajiri duniani yaliyoendelea katika sekta za viwanda, Kilimo, uhandisi, afya, Elimu, sanaa na biashara. Ziara hii ya Rais Samia inatarajiwa kufungua fursa zaidi pamoja na kuyaleta karibu mataifa ya Tanzania na Uturuki.
Rais Erdoghan alitembelea Tanzania wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano na kupolekelewa na aliyekuwa Mwenyeji wake Hayati John Pombe Magufuli wakati Rais Samia akiwa Makamu wa Rais.
Tanzania ina mengi ya kujifunza kutoka Uturuki kwa ajili ya maendeleo yake hivyo ziara ya Rais Samia nchini humo inatarajiwa kuwa na tija kubwa sana kwa Taifa na wananchi wake
Kwenye ziara hii pia, Seneti ya Chuo Kikuu cha Ankara ambacho ni cha pili kwa ukubwa nchini Uturuki chini ya Mkuu wa Chuo hicho Profesa Necdet Unuvar imeamua kwa kauli moja kumtunuku Rais Samia Suluhu Hassan Shahada ya Udaktari wa Heshima (Honoris Causa) kwa kutambua jitihada zake kubwa za kuendeleza mageuzi ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kupitia mtindo wake wa uongozi unaoamini katika 4R.
Amesema uamuzi huo ni kutambua uongozi wa kipekee wa Rais Samia katika kuendeleza mageuzi ya kijamii, kisiasa na kiuchumi nchini Tanzania.
Mageuzi hayo yameboresha ustawi wa Watanzania, kukuza sifa ya Tanzania duniani kote na kuendeleza uhusiano wa kibiashara, kiuchumi na kisiasa kati ya Tanzania na nchi nyingine, ikiwemo Uturuki.
Si jambo linalotokea mara nyingi kwa kiongozi mmoja ndani ya Taifa kutunukiwa Shahada 4 za Heshima kwa mpigo ndani ya muda mfupi wa uongozi wake. Wote tunakumbuka Hayati Rais Magufuli wakati wa uongozi wake wa Awamu ya 5 alitunukiwa mara moja Shahada ya Heshima na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mwaka 2019 na Mstaafu Rais wa Awamu ya 4 Jakaya Kikwete pia mwaka 2011 alitunukiwa mara moja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Akiwa na miaka mitatu pekee, tayali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Shahada 4 za Heshima (Honoris Causa) na Vyuo Vikuu mbalimbali ndani na nje ya nchi. Walianza UDSM Novemba 30, 2022 kumtunuku Shahada ya Juu ya Heshima kwenye Humanitia na Sayansi Jamii (Social sciences), Oktoba 10, 2023 wakafuata Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India na wiki hii Desemba 28, 2023 Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) kumtunuku Shahada nyingine ya Uzamivu ya Usimamizi wa Utalii na Masoko (Doctor of Philosophy in Tourism Management and Marketing- Honors Causa).
Na leo Chuo Kikuu kikubwa cha Ankara cha nchini Uturuki kimentunuku tena Rais Samia Udaktari wa Heshima.
Kwa miaka ya karibuni, anakuwa Rais wa kwanza wa kizazi kipya wa Tanzania kutunukiwa Shahada ya Heshima na Chuo kikubwa chenye heshima kubwa duniani cha Jawaharlal Nehru cha India huku akiandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa Shahada ya Heshima na Chuo hicho na Rais wa 3 pekee baada ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin pamoja ya Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan Hayati Shinzo Abe kutunukiwa na Chuo hicho.
Ndani ya miaka mitatu, Rais Samia ameshatunukiwa Shahada 4 za Udaktari wa Heshima pamoja na Tuzo na kutajwa kwa zaidi ya mara 5 kutoka kwa majarida na taasisi mbalimbali kubwa za kimataifa kwa kutambua kazi yake kubwa anayoifanya kusukuma maendeleo kwenye Taifa lake.
Tayali Jarida maarufu la Avance Media la Ghana lilimtaja kama mmoja wa Wanawake 100 wa Afrika wenye nguvu na ushawishi mkubwa Barani Afrika kabla ya Majarida mengine makubwa yanayosomwa duniani kote kama The Time na Forbes ya Marekani kumtaja pia miongoni mwa Wanawake 100 wenye nguvu ulimwenguni huku Chama Cha Waandishi wa Habari za Miundombinu na Fedha Afrika (MIFA) wakimchagua na kumpa Tuzo pia Rais Samia kama Rais aliyefanya mapinduzi makubwa zaidi ya miundombinu Barani Afrika kwa mwaka 2022.
JE, SHAHADA YA HESHIMA INA MAANA GANI
Shahada ya Heshima ya Falsafa ni Shahada ya Juu sana katika elimu inayotolewa na Taasisi ya Elimu ya Juu (Chuo Kikuu) bila ya kumhitaji Mtunukiwa wa Shahada hiyo kufuata utaratibu wa kawaida na uliozoeleka wa kupata Shahada. Utaratibu wa kawaida kupata Shahada ni mtu kuingia darasani kwa muda wa miaka fulani akisoma na kupikwa na baadae akifaulu hutunukiwa Shahada hiyo. Lakini, Shahada hii haimhitaji Mtunukiwa kuingia darasani.
Hii ni Shahada inayotunukiwa ama kutolewa kwa mtu aliyefanya jambo kubwa, la muhimu na lililoacha alama na kubadilisha maisha ya watu kwenye jamii ama Taifa. Jambo hilo linaweza kuwa kwenye sekta ya elimu, kutumia maarifa yake kutatua changamoto kwenye jamii, kulinda na kupigania haki za binadamu n.k.
Kwahiyo, pindi mtu huyo anapofanya jambo ama harakati iliyoleta mabadiliko makubwa kwenye Jamii au Taifa lake, hutunukiwa Shahada hii kama njia ya kutambua mchango na jitihada zake. Jopo la Wasomi na Wanataaluma kwenye Chuo husika kupitia kwa Baraza, Seneti ama Uongozi wa Chuo husika hukaa na kupendekeza utoaji wa Shahada hiyo ya Heshima kwa mtu huyo aliyeonekana kukidhi vigezo kwa mambo yake makubwa aliyoyafanya.
Hivyo, ili mpaka Maprofesa, Wasomi na Wanazuoni wakubaliane kumtunuku mtu Shahada hii ni lazima kweli mtu huyo awe amefanya kazi kubwa inayotambulika na kuacha alama kwenye jamii, iliyoleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi, kijamii, kielimu, kisiasa, kitamaduni n.k.
Tamaduni na asili ya kutoa Shahada hii ya Heshima ilianza miaka ya 1470 kwenye kipindi cha kati cha zama za ‘Enlightenment’ Barani Ulaya na Marekani kwa Vyuo Vikuu mbalimbali kama Chuo Kikuu cha Oxford na Cambridge kuanza kuandaa utaratibu wa kuwatunuku watu mbalimbali waliokuwa na mchango mkubwa wa kuleta mageuzi katika Jamii.
Mtu wa kwanza kutunukiwa Shahada hii alikuwa Lionel Woodville ambaye alisifika kwa uhodari wake wa kutangaza neno la Mungu na kuuasa ulimwengu kuachana na maasi. Kuanzia hapo sasa, ikawa ndiyo mwanzo wa Shahada hii ya Heshima.
Ikumbukwe, Shahada hii ya Heshima haitolewi tu kienyeji kwa matakwa ya mtu fulani iwe kwa cheo chake ama nguvu ya kifedha bali hufuata utaratibu mrefu wa majadiliano ya kina na jopo la Viongozi wa Chuo husika na Mabaraza yao (Deans).
Vyuo Vikuu vingi vya Marekani, Uingereza, Australia na kote Duniani vimekuwa vikitoa Shahada hii ya Heshima kwa baadhi ya viongozi, wasanii na wengine wote waliotoa mchango mkubwa wa mabadiliko kwenye jamii.
Chuo Kikuu cha Harvard, moja ya vyuo vikubwa duniani kiliwahi kumtunuku Baba wa Taifa la Afrika Kusini Komredi Nelson Mandela mwaka 1998, Wasanii wakubwa wa Marekani kama Kanye West, John Legend, P Diddy, Ben Affleck na Mtangazaji Oprah Winfrey wamewahi pia kutunukiwa Shahada hii ya Heshima. Hata Mtaalamu wa akili wa Ujerumani Albert Einstein nae amewahi kutunukiwa na Chuo Kikuu cha Harvard mwaka 1935.
Vyuo vyote 4 vilivyomtunuku Rais Samia Shahada hizi za Heshima wameeleza kwa kina sababu za kumtunuku.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwenye taarifa yao wameeleza msululu wa mambo yaliyowasukumu kumpendekeza Rais Samia kupata Shahada hii. Kipindi cha uongozi wake madarakani toka aapishwe Machi 19, 2021 pamoja na msululu wa historia ya maisha ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye utumishi wa umma toka miaka ya 1980 akianza na cheo cha chini kabisa kama Karani wa masjala na zaidi kwenye shughuli za kisiasa alizozianza toka miaka ya 2000, imekisukuma Baraza na Seneti ya UDSM kumtunuku Shahada hii.
Historia ndefu ya Uongozi iliyojaa utumishi wa kutosha ndani na Nje ya mipaka ya Tanzania akifanya kazi serikalini, kwenye mashirika ya kimataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) imechangia pakubwa na alama kubwa kwenye Taifa, akiweka historia ya kuwa Mwanamke wa kwanza kushika hatamu kubwa za Kisiasa kwenye Taifa letu akianzia kuwa Makamu wa Rais 2015-2021 na baadae Rais wa Tanzania kuanzia mwaka 2021 mpaka sasa huku akiwa pia Mwanamke wa kwanza kuwa Mwenyekiti wa CCM, Chama kinachoongoza Tanzania na moja ya Chama kikubwa na kikongwe Barani Afrika na Duniani kwa ujumla.
Uongozi wake wa Urais umefanya mageuzi makubwa huku pia hata shughuli zake kabla ya kuwa Rais na kuingia kwenye siasa, zikiacha alama kubwa kwenye Jamii na Taifa la Tanzania.
Mageuzi makubwa aliyoyafanya Rais Samia ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake kwenye ustawi wa Jamii ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya Elfu 12 Nchi nzima mwaka 2021/22 ambayo yaliondoa kero ya kukaa chini, kuchelewa kujiunga na masomo kwa wanafunzi zaidi ya laki tano nchi nzima huku mwaka 2022/23 serikali yake ikijenga madarasa mengine zaidi ya elfu nane. Hiyo inaenda sambamba na kuongeza mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kutoka Bilioni 464 hadi 570, kufuta ada kidato cha 5 na 6, kujenga shule zaidi ya 500 nchi nzima na mengine mengi sana kwenye sekta ya elimu.
Hiyo ni pamoja na kuweka msukumo mpya kwenye ujenzi wa Taifa kwa kuliweka Taifa pamoja baada ya kuonekana kuwa na changamoto kadhaa kwenye eneo hili, kuanzisha maridhiano kwenye uwanja wa siasa kwa kuunda Kikosi kazi Maalum cha kushughulikia changamoto zozote za kisiasa ili Taifa lifanye siasa zenye mlengo wa maendeleo huku akiviita vyama vyote vya siasa kukaa pamoja kushughulikia changamoto mbalimbali za kisiasa ikiwemo haki za binadamu, haki za kila Chama, mikutano ya hadhara, suala la katiba mpya, kuongeza uhuru wa watu kutoa maoni yao, kujieleza n.k.
Ujenzi wa uchumi mpya ikiwemo kuweka nguvu kubwa ya kusimamia huduma za kijamii zote na kuzipa fedha nyingi pamoja na ujenzi wa uchumi wa kuvutia uwekezaji mkubwa sana kupitia uboreshaji mkubwa wa Diplomasia ya kiuchumi ambapo ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wake, uwekezaji uliovunja rekodi wa zaidi ya Dola za Marekani Bilioni 3.5 uliingia Tanzania na kutengeneza mazingira ya ajira ya zaidi ya watu Milioni 5.
Uwekezaji huu ulitiwa chachu na uboreshaji wa Diplomasia na mahusiano mazuri na Mataifa ya Nje ambayo yanaendelea kushuka Tanzania kuwekeza kupitia kujitoa kwa Rais Samia binafsi kusafiri Nje ya Nchi kuvuta uwekezaji na kutangaza fursa zilizopo Tanzania ili kivuta ulimwengu kuja kuwekeza.
Nacho Chuo cha Jawaharlal Nehru cha nchini India kupitia kwa Makamu Mkuu wake wa chuo, Prof. Santishree Dhulipudi Pandit alisema chuo hicho kimemtunuku Rais Samia Shahada hiyo ya Heshima kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na India, Diplomasia ya Uchumi, mchango wake katika maisha ya kila siku ya wananchi wa Tanzania na mafanikio yake kikanda na kimataifa.
Kwa upande wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) wakimtunuku Shahada ya Heshima ya Uzamivu ya Usimamizi wa Utalii na Masoko yaani Doctor of Philosophy in Tourism Management and Marketing- Honors Causa kwa kutambua mchango wake mkubwa wa kuinua uchumi wa Zanzibar na sekta ya utalii ambapo kuingia kwake aliiamsha sekta ya utalii iliyodorora baada ya kutokea mlipuko wa Janga la Corona ambapo Watalii walikata kabisa.
Rais Samia alikuja na Filamu maalum iliyorekodiwa kwenye vivutio mbalimbali vya Utalii vya Tanzania na Rais Samia Suluhu Hassan kama Mhusika Mkuu (Tour guider) pamoja na Wahusika wengine kwa ajili ya kutangaza utalii wa Tanzania, uwekezaji, utamaduni wa Tanzania na kuiambia dunia ukweli kuhusu vivutio vyote vilivyopo Tanzania na namna Taifa hili la Afrika Mashariki lilivyobarikiwa na fursa nyingi za uwekezaji na biashara ili sasa waje kutalii na kuwekeza Tanzania.
Baada ya Filamu hiyo ya Royal Tour, Taifa lilipata mafanikio makubwa ya kuwavuta Watalii na Wawekezaji wengi zaidi nchini. Kwa mujibu wa serikali, baada ya Watalii kushuka sana mpaka Laki tisa (9) kwasababu ya Janga la Corona, Filamu ya Royal Tour ilifanikiwa kuongeza idadi ya Watalii mpaka kufikia zaidi ya Milioni 1.4 kwa Tanzania Bara ikiwa ni ongezeko la asilimia 57 huku kwa upande wa Zanzibar Watalii wakitoka Laki tatu (3) mpaka Laki tano (5) huku Tanzania kwa mara ya kwanza kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Watalii (UNWTO) ikishika nafasi ya pili mwaka 2023 kwa kuingiza Watalii wengi Barani Afrika baada ya Ethiopia.
Mapato ya utalii yakiongezeka mpaka kufikia asilimia 93, hali iliyoongeza fursa za ajira na maendeleo makubwa kwa wananchi.
Hiyo ni pamoja na kazi kubwa aliyoifanya toka akiwa Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji kule Zanzibar kutoka mwaka 2005 hadi 2010 ambapo alifanya kazi kubwa ya kusukuma utalii kwa kusafiri mataifa mbalimbali kuwavuta watalii na wawekezaji ambao wengi walifika Zanzibar kujenga hoteli za kisasa na kupaisha zaidi utalii wa Zanzibar.
Haya yote pamoja na mengine ambayo sikuyajumuisha yamevisikuma Vyuo vikuu hivi kumtunuku Rais Samia Suluhu Hassan. Je, kuna ubishi tena kuhusu kustahili kwake? Rais Samia anastahili kutunukiwa Shahada hizi kwa kazi kubwa anayoifanya.
Imeandaliwa na Bwanku M Bwanku, Mwandishi wa Habari za Siasa, Uchumi na Maendeleo. Anapatikana kwa namba 0657475347
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani