May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia aipongeza Kilimanjaro, kutii agizo lake

Na Martha Fatael, TimesMajira online

RAIS Samia Suluhu Hassan amepongeza viongozi wa mabakabila na kimila mkoani Kilimanjaro kwa kuwa mkoa wa kwanza kutekeleza maagizo yake ya kufanya tamasha la utamaduni kwa kila mkoa.

Rais Samia alitoa maagizo hayo tarehe 8 September 2021 akiwa Mkoani Mwanza Mara baada ya kusimikwa kuwa kiongozi mkuu wa makabila na kupewa jina la Hangaya.

Amesema alitoa maagizo hayo ili kuendeleza na kuimarisha utamaduni wetu utakao tutambulisha kimataifa kama watanzania lakini pia kwa pamoja kuandaa matamasha mbalimbali ya kitamaduni na kimila kila mara.

“Natambua Kuna maandalizi ya tamasha kubwa litakalofanyika mwezi Mei mwaka huu, naagiza kuwepo na ushirikishwaji mzuri wa machifu na wale viongozi wa kimila ili likawe tamasha kubwa na la kihistoria…..pasiwepo na kutoshirikishwa kwa kila hatua kwa viongozi Hawa nchi nzima” amesema

Aidha Rais Samia amesema tayari serikali imeanza hatua za kuwasajili machifu nchini ambapo zaidi ya machifu 92 tayari wamesajiliwa hadi kufikia Januari 20 mwaka huu huku maeneo 36 ya kihistoria yakiorodheshwa na bado utaratibu unaendelea.

“Tutaendelea kushirikiana kutunza na kuyahifadhi maeneo hayo ya kihistoria ili yasivamiwe wala kuharibiwa na tutaendelea kuimarisha bajeti ya wizara husika ili muweze kufikia malengo yenu mliyojiwekea kwa kushirikiana na serikali” amesema

Kadhalika Rais Samia ametoa pole kwa wananchi kwa majanga mbalimbali ikiwemo la kufa kwa mifugo kutokana na kukosa malisho hususan mikoa ya Manyara na Arusha huku akiwataka wananchi pia kuhifadhi chakula ili kuepuka kujitokeza kwa janga jingine la njaa.

Akitoa taarifa kwa Rais Samia, mkuu wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai amesema wamepokea zaidi ya Bil. 47 kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa madarasa, barabara, afya na miradi mingine ya maendeleo.

Amesema miongoni mwa fedha hizo zipo fedha za Uviko 19 zaidi ya Bil 7 ambazo zimetumika kujenga madarasa 27 huku shule 9 mpya za kata zikianza ujenzi wake katika hamashauri za mkoa huo.

Kagaigai amesema kwa sasa Kuna miradi zaidi ya 28 ya ujenzi wa miundombinu ya barabara inayoendelea kwa hatua mbalimbali za matengenezo ya kawaida na ukarabati miradi iliyopo chini ya wakala wa barabara nchini(TARURA) na wakala wa barabara Tanzania (TANROADS).

Awali mwenyekiti umoja wa machifu Tanzania (UMT), Mangi Frank Marialle ameomba serikali kupitia wizara ya utamaduni na michezo kuanzisha mfumo wa ukusanyaji taarifa na kuhifadhiwa na ofisi ya taifa ya takwimu(NBS) ili ziweze kutumika kwenye kumbukumbu za kihistoria za nchi.

Amesema ni vyema ukaanzishwa utafiti rasmi wa maeneo, majengo na viongozi wa kimila na makabila waliosaidiana katika kupigania uhuru wa nchi ili maeneo na nyumba hizo zihifadhiwe na kutumika kuwafundishia vijana lakini pia kuwa sehemu ya utalii.

“Tunaanzisha utaratibu wa kufufua ushirikiano baina ya viongozi wa makabila na kimila ili kwa pamoja tuisaidie serikali katika kukuza na kuendeleza Mila na tamaduni zetu zilizo njema ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye shughuli muhimu za maendeleo kama utunzaji wa mazingira” amesema Marialle

Kwa upande wake naibu waziri utamaduni, sanaa na michezo Pauline
Gekul amewaomba viongozi hao wa makabila na wa kimila kuisaidia serikali kufuta Mila zinazoumiza na zisizo na matokeo chanya kwa jamii.