April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tigo kili half marathon 2022 yazinduliwa Moshi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kampuni ya Tigo imedhamini tena mbio hizi maarufu za Tigo Kili Half Marathon (Km 21) ikiwa ni mara ya saba mfululizo, ili kutoa fursa kwa watanzania na watu kutoka nchi jirani kushiriki, kubadilishana tamaduni,kuburudika na kufurahi kwa pamoja.

Mbio hizo za Kilimanjaro Marathon 2022 zitafanyika mkoani Kilimanjaro, Mjini Moshi ambako ni mojawapo wa kitovu kikubwa cha shughuli za kiuchumi ikiwemo utalii

Akizungumza katika uzinduzi wa mbio hizo, Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini Henry Kinabo amesema mwaka huu wamejipanga kufanya mambo mengi zaidi kwaajili ya mradi wa Tigo Green For Kili kwani muamko kutoka makampuni mbalimbali na wadau mbalimbali umekua mkubwa;

“Mwaka jana tulizindua mradi wetu wa Tigo Green for Kili,ulio kuwa na dhamira ya kuboresha mazingira na kurudisha theluji katika Mlima Kilimanjaro,mradi huu endelevu ukiwa na lengo la kupanda miche 28,000. Mwaka huu tumejipanga kufanya mengi zaidi kwaajili ya mradi huu kwani muamko ulikuwa mkubwa sana kutoka kwa makampuni na wadau mbali mbali.”

Aidha Kinabo amewakumbusha watanzania wote ambao wangependa kushiriki kwenye mbio hizo za Tigo Kili Half Marathon kujisajili mapema ili waweze kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kushiriki.

Amesema dirisha la usajili kwaajili ya Tigo Kili Half Marathon 2022 pamoja na mbio za Km 42 na Km5 limekwisha kufunguliwa na wateja wa Tigo wanaweza kupiga 14920# ili kujisajili na kufanya malipo.

Aidha Kinabo amesema Ili kujisajili,mteja wa Tigo atatakiwa kupiga 14920# kisha kuchagua aina ya mbio anazotaka kushiriki na kufuata maelekezo kwaajili ya kufanya malipo na baadaye atapokea ujumbe wa kuthibitisha malipo yake.

Kinabo ameongeza kuwa Mshiriki wa mbio hizi anatakiwa kuhifadhi ujumbe (SMS) na atatumia kama uthibitisho akiambatanisha na kitambulisho chake wakati wa kuchukua namba ya ushiriki katika vituo vilivyopo Dar es Salaam, Arusha na Moshi.

Kinabo amesema katika mbio hizo Tigo watatoa zawadi mbalimbali kwa washindi;

“Katika mbio hizi, Tigo inatoa zawadi za kifedha zenye thamani ya Shilingi Milioni 12.5 kwa washindi 10 wa kwanza wa Tigo Kili Half Marathon (wanawake na wanaume).Pia,washiriki 4,500 watakaomaliza Km 21 watapewa medali za heshima.Vilevile, tutatoa vyeti kwa washiriki wote wa Tigo Kili Half Marathon.”

Kampuni ya Tigo imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha utalii kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo kudhamini mbio za nusu marathoni maarufu kama Tigo Kili Half Marathon (21).