January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Magufuli awateua Dkt. Shein kuongoza Mzumbe, Dkt. Mwakyembe MUHAS

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS John Magufuli amefanya uteuzi wa viongozi watatu, ikiwemo kumteua Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe.

Dkt. Shein anachukua nafasi ya Jaji Mstaafu Barnaba Samatta ambaye anamaliza muda wake.

Taarifa iliyotolewa leo na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, imewataja wengine walioteuliwa kuwa ni Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).

Dkt. Mwakyembe anachukua nafasi ya Mariam Mwaffisi ambaye amemaliza muda wake.

Aidha, Rais Magufuli amemteua, Gaudentia Kabaka kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Kabaka anashika wadhifa huo kwa kipindi cha pili baada ya kipindi cha kwanza kumalizika.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo uteuzi wa viongozi hao umeanza jana.