May 13, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt. Samia kuja na mfuko wa kusaidia wafungwa wanaomaliza vifungo

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan amesema ipo haja ya kuanzishwa kwa mfuko maalumu utakaowasaidia wafungwa wanaomaliza vifungo kuanza maisha mapya mara wanaporejea katika jamii.

Dkt Samia ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam mapema leo Mei 9,2026 alipokuwa akihitimisha mafunzo ya uongozi ngazi ya juu kozi namba 28 na uongozi daraja la pili kozi namba 48 kwa mwaka 2025/2026 kutoka Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA) kilichopo Ukonga jijini Dar es Salaam.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza kurejea kwao tena magerezani kutokana na changamoto za kiuchumi.

“Nimetembelea maonyesho ya kazi mbalimbali zinazofanywa na wafungwa, nimejionea kiwango kikubwa cha ujuzi unaotolewa na magerezani ikiwemo ushonaji, useremala, utengenezaji wa viatu na shughuli nyingine za uzalishaji zenye uwezo wa kuwasaidia kujitegemea”amesema Dkt Samia

Amesema changamoto kubwa inayowakabili wengi wao ni ukosefu wa mtaji wa kuanzia mara wanapomaliza vifungo, hali inayowafanya baadhi yao kushindwa kutumia ujuzi walioupata na hivyo kurejea katika mazingira ya kufanya makosa.

Hivyo amewataka viongozi wa Jeshi la Magereza kuanzisha sera ya namna ya kuanzisha mfuko maalum wa kuwawezesha wafungwa wanaotoka magerezani kwa kuwapatia mtaji wa awali wa kuanzisha shughuli za uzalishaji na kujitegemea.

Katika hatua nyingine Dkt Samia amesema wanawake walioko magerezani wanapaswa kuthaminiwa na kuheshimiwa utu wao licha ya kuwa wanatumikia vifungo kutokana na makosa mbalimbali.

Amesema ni muhimu kwa askari wa Jeshi la Magereza kuhakikisha wafungwa wanawake wanapata haki zao za msingi na kushughulikiwa kwa kuzingatia utu na staha wanapokuwa wakitumikia adhabu zao.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Nchini, Jeremiah Katungu aliishukuru serikali kwa kuendelea kuliwezesha jeshi hilo kupitia ongezeko la bajeti, ajira mpya na maboresho ya vitendea kazi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amepongeza maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali katika Jeshi la Magereza, akisema hatua hiyo imeongeza ufanisi wa utendaji na kuimarisha taswira ya vyombo vya dola nchini.

Awali Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amemshukuru Rais Dk.Samia kwa maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika katika vyombo vya usalama nchini.