May 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Dkt.Mwinyi alipongeza Kanisa la Anglikana kuendeleza amani nchini

Na Mwandishi wetu, timesmajira

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amelipongeza Kanisa la Anglikana Tanzania kwa kuendeleza amani, umoja na mshikamano nchini.

Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo leo alipokutana na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Maimbo Mndolwa na ujumbe wake waliofika Ikulu Zanzibar kujitambulisha baada ya kuchaguliwa mwezi Februari mwaka huu kuliongoza Kanisa hilo kwa kipindi cha miaka mitano.

Aidha Rais Dk.Mwinyi amewashukuru viongozi wa kanisa hilo kwa mipango yao ya kuitangaza Zanzibar katika sekta ya utalii na Serikali ipo tayari kuendeleza ushirikiano na kanisa katika sekta hiyo.

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Maimbo Mndolwa amempongeza Rais Dk.Mwinyi kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Vilevile Askofu Mndolwa amesema kanisa linaendelea kumuombea katika uongozi wake.