November 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais agawa wizara,ateua mawaziri wapya

Na Mwandishi Wetu 

RAIS wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko ya muundo wa Wizara mbili (2), uteuzi na uhamisho wa viongozi mbalimbali ili kuimarisha utendaji wa Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Novemba 25,2026 na  Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka,Rais amegawanya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa Wizara mbili ambazo ni  Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Pia amegawanya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa Wizara mbili ambazo ni Wizara ya Mifugo  na Wizara ya Uvuvi.

Hata hivyo  Rais amemteua Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kabla ya uteuzi  Balozi Kombo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.) ameteuliwa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kabla ya uteuzi Kairuki alikuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

Aidha Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Mb.) ameteuliwa kuwa Waziri wa Mifugo. Kabla ya uteuzi huu,Balozi Dkt. Kakurwa alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.Huku Hamis Mohamed Mwinjuma (Mb.) ameteuliwa kuwa Waziri wa Uvuvi. Kabla ya uteuzi huu,Mwinjuma alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Sanjari na hayo Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe (Mb.) ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kabla ya uteuzi Dkt. Maghembe alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Vilevile James Kinyasi Millya (Mb.) ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ushirikano wa Afrika Mashariki. Kabla ya uteuzi Millya alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Kadhalika Ng’wasi Damas Kamani (Mb.) ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo. Kabla ya uteuzi huu, Mhe. Kamani alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.Huku Subira Khamis Mgalu (Mb.) ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Uvuvi.