Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza
SERIKALI imesema ajali ya meli ya MV Mwanza kugonga mwamba ndani ya Ziwa Victoria imesababishwa na makosa ya kibinadamu, baada ya uchunguzi kubaini kuwa wataalamu hawakuwa na uzoefu wa kutosha wa kuendesha mitambo ya kisasa ya meli hiyo.
Kutokana na ajali hiyo Serikali imeagiza hatua za kinidhamu, kitaaluma na kisheria kuchukuliwa dhidi ya nahodha, wataalamu na viongozi walioshindwa kutimiza wajibu wao.
Aidha, imesisitiza kuwa injini na mifumo ya meli hiyo iko salama na haikupata athari, huku ikiwatoa hofu wananchi na kuwataka kuwa watulivu na kuepuka taarifa potofu za mitandao ya kijamii.
Hayo yameelezwa leo Novemba 26,2026 ikiwa ni siku ya nane tangu kutokea kwa ajili hiyo na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa,wakati akitoa taarifa ya uchunguzi wa ajali hiyo, iliyotokea Novemba 18, mwaka huu, majira ya saa 4 asubuhi, wakati meli ikiwa katika safari ya majaribio kutoka Bandari ya Mwanza Kusini kuelekea Mwanza Kaskazini.
Hata hivyo itakubukwa kuwa wakati akitoa taarifa ya awali juu ya ajali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza CP.Salum Hamduni alisema kuwa uchunguzi utafanyika ndani ya siku 14 na wananchi watapata taarifa ya kile kilichobainika.
“Napenda kuufahamisha umma kuwa, hakuna mtu aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa, hakuna uchafuzi wa mazingira uliotokea kutokana na ajali hiyo. Baada ya tukio hilo meli ya MV Mwanza iliweza kurejea Bandari ya Mwanza Kusini kwa kutumia injini zake yenyewe bila kuhitaji msaada wa chombo kingine,”amesema Prof.Mbarawa.
Prof.Mbarawa amesema,kutokana na umuhimu wa usalama wa usafiri wa majini na thamani ya uwekezaji huo kwa Taifa,Serikali ilichukua hatua za haraka kwa kusimamisha uendeshaji wa meli hiyo na kuanzisha uchunguzi wa kitaalamu.
Amesema, Serikali ilielekeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kusimamisha shughuli za uendeshaji wa meli hiyo na kuunda timu ya wataalamu kuchunguza chanzo, mazingira ya ajali, kiwango cha uharibifu na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Timu hiyo ilihusisha wataalamu wa usanifu wa ujenzi wa meli, wahandisi wa mitambo ya meli na wataalamu wa uendeshaji wa vyombo vya majini na uchunguzi wa ajali za meli.Uchunguzi huo ulizingatia misingi na kanuni za kimataifa za uchunguzi wa ajali za meli za uendeshaji wa meli (IMO).
Hata hivyo amesema,uchunguzi ulijikita katika maeneo makuu sita, ikiwemo uongozaji na uendeshaji wa meli, ambapo walichunguza njia ya safari, kasi ya meli, mwelekeo na mpango wa safari, pamoja na matumizi ya vifaa vya uongozaji kama ramani, GPS, rada na “echo sounder”.
Eneo la pili walichunguza mazingira ya safari, maamuzi ya nahodha kabla na baada ya ajali, mfumo wa usukani, mafuta, uongozi wa mikono, mifumo ya dharura na tahadhari.
Katika eneo la tatu, walichunguza mfumo wa udhibiti wa injini na chumba cha kuongozea meli, gia, pangaboi na umeme, huku eneo la nne likihusu mawasiliano ndani ya meli, ufanisi wa mawasiliano kati ya chumba cha kuongozea na chumba cha injini na utekelezaji wa amri.
Prof.Mbarawa amesema,eneo la tano lilihusu sifa za kitaalamu za watumishi, vyeti, leseni, uzoefu, mafunzo na uelewa wa matumizi ya teknolojia ya kisasa ya meli hiyo, pamoja na kubaini uzembe huku eneo la sita lilihusu ukaguzi wa muundo na chini ya meli, ambapo wazamaji na wataalamu walizamia kubaini athari zilizotokana na ajali hiyo.
“Uchunguzi haukubaini hitilafu katika injini na mifumo ya kuongozea meli, bali makosa ya kibinadamu yaliyotokana na nahodha kushindwa kutimiza wajibu wake kwa umakini.Hivyo Serikali imeagiza TASHICO kumsimamisha kazi nahodha wa meli hiyo kwa makosa ya uzembe huku wataalamu na viongozi watakaobainika kutotekeleza wajibu wao wakichukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria,”amesema Prof.Mbarawa.
Vilevile amesema,Serikali itaendelea kulinda uwekezaji huo ili wananchi wapate huduma bora, akisisitiza kuwa usalama wa Watanzania hautakuwa jambo la majadiliano, bali msingi muhimu wa usafiri wa majini kwa viwango vya kimataifa.

More Stories
Wananchi waaswa kujitokeza maadhimisho siku ya UKIMWI
ARMFA yapokea programu ya kulinda mapato ya barabara
Vijana wahimizwa kutumia fursa za ubia miradi ya nishati