Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Tanga
NABII Mkuu Nicholous Suguye ametoa wito kwa Watanzania wenye uwezo kujenga utamaduni wa kusaidiana kwa kuwafikia watoto yatima, wajane na makundi mengine yenye uhitaji katika jamii, akisisitiza kuwa kutoa msaada si suala la kuwa na utajiri mkubwa, bali ni moyo wa upendo na utayari wa kushirikiana na wenye mahitaji.
Kauli hiyo ameitoa jijini Tanga wakati wa ziara yake ya kutembelea vituo viwili vya kulelea watoto yatima vya Goodwill Children Home na Nyumba ya Furaha ya Casa de la Familia, ambapo amekabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali kwa ajili ya kuboresha ustawi wa watoto wanaolelewa katika vituo hivyo.

Katika ziara hiyo,Nabii Suguye amekabidhi vyakula, nguo, viatu, mafuta na magodoro, huku akitangaza kuongeza mchango wa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba ya watoto, hatua inayolenga kuchangia kuboresha mazingira ya makazi na malezi kwa watoto hao.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Suguye amesema,kuwajali watu wenye uhitaji ni sehemu muhimu ya kutekeleza mafundisho ya dini, ambayo yanahimiza upendo, huruma na kuwasaidia watu wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha.
Amesema kabla ya kufanikisha zoezi hilo, walifanya mazungumzo na viongozi wa vituo hivyo ili kufahamu changamoto na mahitaji yaliyokuwa yanawakabili, ambapo walibaini kuwepo kwa mahitaji muhimu yakiwamo magodoro na viatu kwa ajili ya watoto.
Amefafanua kuwa baada ya kupata taarifa hizo, waliamua kutumia sehemu ya sadaka zilizotolewa kwa ajili ya Mungu kununua mahitaji hayo na kuyafikisha moja kwa moja kwa watoto wanaoyahitaji.
Hata hivyo amesema,walipofika katika vituo hivyo walibaini kuwa mahitaji ni makubwa zaidi kutokana na idadi ya watoto wanaohitaji malezi na huduma mbalimbali, hali iliyowafanya waone umuhimu wa kuongeza mchango wao ili kusaidia kupunguza changamoto zinazowakabili walezi.
Ameeleza kuwa katika kituo kimoja pekee idadi ya watoto wanaolelewa inafikia 85, jambo linaloonesha ukubwa wa jukumu lililonalo kituo hicho katika kuhakikisha watoto wanapata mahitaji muhimu ya kila siku.
Kutokana na hali hiyo,Nabii Suguye amesema,msaada walioutoa haupaswi kuishia kuwa tukio la siku moja, bali uwe sehemu ya mwamko mpana wa jamii kutambua wajibu wa kushirikiana katika kuwasaidia watoto wanaokosa huduma muhimu za malezi na mahitaji ya msingi.
Amesisitiza kuwa watu wengi wanaweza kushiriki katika kusaidia jamii kulingana na uwezo wao, akieleza kuwa hata mchango mdogo unaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa mtu anayekabiliwa na uhitaji.
“Si lazima uwe tajiri mkubwa ili uweze kusaidia. Kila mtu anaweza kutoa kile kidogo alichonacho kupitia mikono ya yatima na wajane. Unachotoa leo kinaweza kuwa kidogo kwako, lakini kwa anayekipokea kina maana kubwa,”amesema Suguye.

Ameongeza kuwa lengo la kufanya ziara hiyo na kutoa misaada si kujitangaza, bali ni kuonesha mfano na kuhamasisha watu wengine, taasisi na wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia vituo vya watoto yatima na makundi mengine yanayohitaji msaada.
Amesema jamii inapaswa kujenga utamaduni wa kutembeleana, kufuatilia hali za watu wenye uhitaji na kuchangia katika kuboresha maisha yao, badala ya kusubiri matatizo yao yawe makubwa ndipo hatua za kuwasaidia zichukuliwe.
Kwa mujibu wa Suguye, upendo wa kweli hauishii katika maneno pekee, bali unapaswa kuonekana kupitia matendo yanayogusa maisha ya wengine, hususan watoto ambao wanahitaji mazingira bora ya kukua, kupata malezi na kujenga matumaini ya maisha yao ya baadaye.
Katika hatua nyingine,Nabii Suguye ametangaza kuendesha huduma maalumu ya maombi na maombezi mkoani Tanga kuanzia Jumatano, Novemba 25 hadi Jumapili, ikiwa na lengo la kuwafikia watu wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za maisha.
Amesema huduma hiyo itatoa nafasi kwa watu wenye mahitaji tofauti kujumuika katika maombi, akitaja changamoto zinazohusiana na magonjwa, umaskini na matatizo mengine ambayo baadhi ya waumini huyatafsiri kuwa yanahusiana na masuala ya kiroho.
Alieleza kuwa katika huduma yake amekuwa akikutana na watu wanaopitia mazingira magumu ya maisha, ambao kwa mtazamo wake wanahitaji pia faraja, ushauri na msaada wa kiroho ili kuimarisha imani na matumaini yao.


More Stories
Makosa ya kibinadamu chanzo MV Mwanza kugonga mwamba
Wananchi waaswa kujitokeza maadhimisho siku ya UKIMWI
ARMFA yapokea programu ya kulinda mapato ya barabara