Na Mwandishi Wetu Timesmajira Online
Puma Energy Tanzania imezindua kituo chake cha kwanza cha rejareja cha Gesi Asilia iliyoshindikizwa (CNG) kilichopo Tangi Bovu, Barabara ya Bagamoyo, jijini Dar es Salaam, hatua inayoweka kampuni hiyo katika mstari wa mbele wa kutoa suluhu za kisasa za nishati nchini.
Hafla ya uzinduzi huo imehudhuriwa na Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi J. Mramba, pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, Kaimu Balozi wa Canada, Carol Mundle, na viongozi waandamizi wa kampuni hiyo.
Kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha gesi zaidi ya milioni moja za futi za ujazo kwa siku na kuhudumia magari madogo, makubwa na bajaji Kimewekewa mashine mbili za kisasa zenye uwezo wa kuhudumia magari 50 kwa saa, compressor kutoka Canada yenye nguvu ya 250 HP na hifadhi ya gesi ya lita 4,000, hatua inayolenga kuhakikisha huduma inapatikana bila kukatika hata wakati wa mahitaji makubwa.

Aidha, kituo cha Bagamoyo Road kimeboreshwa kwa huduma jumuishi, kikiunganisha utoaji wa gesi asilia (CNG) pamoja na petroli, dizeli, LPG, vilainishi na duka dogo, na hivyo kuwa kituo cha kisasa na cha huduma kamili kwa madereva na wafanyabiashara, Pia kimewekewa mfumo wa ukaguzi wa ubora wa gesi unaolinda usalama na kuongeza ufanisi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Fatma Abdallah amesema uzinduzi wa kituo hicho ni mwanzo wa mageuzi makubwa katika sekta ya nishati nchini. “Tuna furaha kuanzisha miundombinu ya kisasa inayopunguza uzalishaji wa hewa ya kaboni na kutoa huduma ya uhakika kwa wateja. Muhimu zaidi, huu ni mwanzo—tuko tayari kufungua vituo zaidi kabla ya mwisho wa mwaka huu,” amesema.
Kwa upande wake, Emmanuel Bakilana, Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Masuala ya Kampuni, amesisitiza dhamira ya Puma Energy katika usalama na ubora wa huduma. “Wateja wetu wanaweza kuitegemea Puma kwa usalama, ubora na upatikanaji wa uhakika. Kituo hiki kinaonyesha uwekezaji wetu katika miundombinu ya kisasa na nafasi yetu kama kinara wa suluhu rafiki za usafirishaji,” ameeleza.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako