May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PSSSF yatahadharisha wastaafu kuhusu matapeli

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umewataka wanachama wastaafu wa mfuko huo kuwa makini na matapeli kutokana na kuwepo kwa wimbi kubwa la watu hao.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam leo kikao kazi baina ya mfuko huo na wanachama wa Chama cha waandishi wa habari Dar es salaam ( DCPC), Meneja wa Uhusiano na Elimu Kwa Umma wa PSSSF, James Mlowe, matapeli hao wanatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutoa taarifa zao kwa wahusika wa wizi au matapeli kuwatumia maafisa waajili kutafuta taarifa zao kwa njia za udanganyifu.

“wanachofanya ni kudanganya kwamba wanatoka Tamisemi au sehemu nyingine ya ajira na wanataka taarifa za wastaafu wote na maofisa waajili huwapatia.”

Aidha alitoa wito kwa waandishi wa habari kusaidia kutoa elimu kwa wastaafu kutomtumia mtu yeyote taarifa zake za kustaafu ikiwemo wafanyakazi wa PSSSF.

Alisema mstaafu anapopokea barua ya kustaafu anatakiwa kuanza hatua ya kufuatilia mafao yake kwa kwenda hatua inayofuata ya kufuata fomu ya PSSSF.

Katika hatua nyingine Mlowe alisema kuhusu changamoto za kuchelewa kuwalipa wastaafu zilizokuwepo hapo nyuma alisema ilitokana na kurithi deni la Sh. trilioni moja .

Alisema deni hilo lilitokana na madai ya kulipwa wanachama waliokuwa wametoka kwenye ajira katika mifuko minne iliyounganishwa na kuzaliwa PSSSF.

Aliongeza kuwa changamoto nyingine ilitokana na wanachama kutokamilishiwa michango na waajili wao, hivyo kusababisha kutumia muda kumfuatilia.

Kwa upande wake Katibu wa DCPC Fatma Jalala alisema Chama hicho kitaendelea kushirikiana na PSSSF katika kuhakikisha jamii inapata elimu kuhusu mfuko huo.