NA
K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, DAR ES SALAAM
MFUKO
wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Umepewa tuzo na Taasisi ya
Kimataifa ya Hifadhi ya Jamii (International Social Security Association-ISSA)kutokana
na mafanikio iliyoyapata katika kipindi kifupi baada ya kuunganishwa (Merge)
kwa mifuko minne ya Hifadhi ya Jamii ya PSPF, PPF, GEPF NA LAPF na kuwa PSSSF.
Akizungumzia
tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba alisema sababu nyingine
iliyoifanya ISSA kutoa tuzo kwa Mfuko huo ni pamoja na jinsi Mfuko ulivyoweza
kupunguza gharama za uendeshaji na ulipaji wa mafao kwa wakati.
“Kwenye
suala la kuunganisha mifuko yapo mambo manne ambayo ISSA imeyaona na kuona ni
mafanikio ambayo ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji, kutoa mafao
yanayofanana kwa wanachama wa Mfuko licha ya kutoka kwenye mifuko tofauti,
kukabiliana na madeni kabla ya mifuko kuunganishwa na pia suala la uwekezaji
hususan katika viwanda.” Alisema
CPA
Kashimba aliishukuru Bodi ya Wadhamini kwa usimamizi mzuri na hivyo kuufanya
Mfuko huo kufanya vizuri.
“Kazi
kubwa ya kusimamia zoezi hili la kuunganisha mifuko mmeifanya ninyi Bodi kwa
maelekezo ya serikali, sehemu nyingi duniani wanasema karibu asilimia 85 ya
kampuni zilizoungana huwa zinashindwa lakini muunganiko wetu sisi umeendelea
kufanya vizuri hadi kuivutia taasisi hii kubwa kuifanya PSSSF kuwa mfano wa
kuigwa.” Alisema CPA Kashimba.
Alisema
tayari Mfuko umeanza kupokea wageni KUTOKA sehemu mbalimbali wakihitaji kujifunza kutoka PSSSF.
“Juzi
kamati ya bunge ya Uganda wao wanaanzisha Mfuko wa Watumishi wa Umma na walikuja
kujifunza na wameridhishwa na elimu tuliyowapatia.” Alifafanua.
Alisema
tuzo hiyo ni zawadi kwa Bodi na sio Menejimenti pekee na mfuko uko kwenye
mikakati ya kuhakikisha unaendelea kutoa huduma bora kwa Wanachama na Wastaafu
kwa ujumla.
Awali Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF, Bw. Mbarouk Magawa alidokeza kuwa eneo lingine ambalo liliwavutia watoa tuzo ni jinsi mfukoulivyofanya maboresho makubwa katika utoaji wa huduma kwa wastaafu na wanachama.
“Suala la Huduma kwa wananchama, jinsi tunavyokusanya michango, tunavyolipa mafao, kutoka kwenye matumizi ya hundi kulipa mafao, lakini jinsi tunavyohakiki wastaafu wetu, haya yote yaliwavutia.” Alifafanua Bw. Magawa.
Aidha Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma (PSSSF) Bw. James Mlowe alisema PSSSF
ilikabidhiwa tuzo hiyo jijini Abidjan Ivory Coast Mei 17, 2023 na kwamba ifikapo
Agosti Mosi, 2023 PSSSF itafikisha miaka mitano tangu kuundwa kwake baada ya
kuunganishwa kwa mifuko (merge), Agosti Mosi, 2018.
“Majukumu
ya mfuko yanatekelezwa vizuri, uwezo wa mfuko unazidi kuimarika, watumishi
wanazidi kuwa kitu kimoja na kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kwakweli mafanikio
haya ndiyo yamewavutia ISSA kuweza kutoa tuzo hii” Alisema
“Tunajisikia
faraja kwa tuzo hii na hii imekuwa chachu ya kuendelea kutekeleza majukumu yetu sawasawa
kuendelea kuwahudumia wanachama wetu na wastaafu kikamilifu.” Alitoa hakikisho.
Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF, Bw. Mbarouk Magawa, akielezea mchakato uliopelekea PSSSF kupewa tuzo hiyo.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais