May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Mkenda:Wabunifu jitokezeni usajili MAKISATU,sh.1 bilioni yatengwa maadhimisho Ubunifu ,MAKISATU

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online ,Dodoma

SERIKALI imewaasa wabunifu kote nchini kujitokeza katika kujisajili ili waweze kushiriki kwenye maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu na yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Mei 15-20 ,2022 ambayo yametengewa shilingi bilioni moja.

Aidha zaidi ya wabunifu 480 ambao wameshajisajili mpaka sasa wanatarajiwa kushiriki katika maadhimisho hayo ambayo yataenda sambamba na kilele cha mashindano ya Sayansi ,Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) ambapo wabunifu 21 watakaoshinda watapata tuzo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema

,wiki ya maadhimisho hayo Kitaifa itafanyika mkoani Dodoma lakini pia  inatarajiwa kufanyika katika mikoa 17 nchini ambayo Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Arusha, Iringa, Mwanza na  Zanzibar.

Pia inatarajiwa ufanyika mikoa ya  Tanga, Kilimanjaro, Morogoro, Njombe, Kagera, Mtwara, Kigoma, Mara na  Ruvuma.

Aidha Profesa Mkenda alisema,kupitia MAKISATU 2019, 2020 na 2021, Wizara imefanikiwa kuibua na kutambua wabunifu wachanga 1,785 ambapo kupitia wabunifu hao, bunifu 466 zilikidhi vigezo na  zimetambuliwa na kuhakikiwa.

“Aidha kati ya hizo , bunifu mahiri 200 tayari zinaendelezwa na Serikali ili kufikia hatua ya kubiasharishwa. “amesema Profesa Mkenda na kuongeza kuwa

“Kati ya bunifu zinazoendelezwa na Serikali, 26 zimeshafikia hatua ya kubiasharishwa, huku  95 zikiwa  katika hatua ya Sampuli kifani  na nyingine zipo katika hatua za awali za kuandaa sampuli kifani. “

Waziri Mkenda Ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wabunifu kote nchini  kutumia fursa hiyo  ili ubunifu wao  uweze kutambulika, kuendelezwa na hatimae kutumika katika shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akifafanua zaidi Waziri Mkenda amesema,wiki ya Ubunifu na MAKISATU zinalenga, pamoja na mambo mengine, kuibua, kutambua na kuendeleza jitihada zinazofanywa na wabunifu wa Kitanzania na kuhamasisha matumizi ya Sayansi Teknolojia na ubunifu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, kupitia maonesho ya bidhaa wakati wa Wiki ya Ubunifu, wabunifu watapata nafasi ya kujitangaza na bidhaa zao kujulikana kwa watumiaji na wadau wengine.

Alisema,maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu yatahusisha pia majukwaa na majadiliano kuhusu maendeleo ya Sayansi, teknolojia na ubunifu Nchini, mafunzo na semina kwa wabunifi ikiwemo elimu ya ujasiriamali.

“ Aidha, mijadala hiyo itawahusisha wabunifu, wadau mbalimbali wa ubunifu na Serikali, kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kuhamasisha matumizi ya teknolojia na ubunifu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.”alisema

Kwa upande wa Mashindano ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, washiriki watatoka katika makundi saba ambayo ni  Shule za Msingi, Shule za Sekondari, Vyuo vya Ufundi Stadi,Vyuo vya Ufundi,Vyuo Vikuu,Taasisi za Utafiti na Maendeleo, na Mfumo usio Rasmi.

Aidha amesema,usajili wa ubunifu kwa ajili ya ulianza Disemba 27 mwaka jana na ilikuwa ni Februari 10 ,mwaka huu lakini hata hivyo kutokana na  uhitaji, muda wa usaji umeongezwa hadi Februari 28 mwaka huu .

“Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa wabunifu Nchini kuendelea kujisajili ili kushiriki MAKISATU 2022….,mwongozo na fomu za maombi ya kushiriki zinapatikana katika tovuti za Wizara na Taasisi zake na usajili wa washiriki unafanyika kupitia tovuti ya MAKISATU: http//makisatu.costech.or.tz.