May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof Bengesi:Tanzania haitakuwa na uhaba wa sukari ifikapo 2025/26

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

SERIKALI kupitia Bodi ya Sukari Tanzania imesema kuwa Nchi haitakuwa na uhaba wa sukari katika kipindi Cha Mwaka 2025/2026 ambapo uzalishaji utaongezeka kutoka Tani laki 3 na 80 za Sasa hadi kufikia Tani laki 7 na 56 elfu.

Hayo yameelezwa jijini hapa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania,Prof.Keneth Bengesi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa Majukumu ya Bodi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Prof.Bengesi ameeleza kuwa  Serikali imekuwa inatumia zaidi ya Dolla Million 150 ambazo ni zaidi ya Sh.Billion 300 ya fedha za Kitanzania kuagiza sukari toka nje ya nchi kila Mwaka ambapo huagiza Tani laki 6 na 45 elfu za Sukari ya matumizi ya kawaida na matumizi ya Viwandani.

Kutoka na hilo amesema kuwa Uhaba huo wa Sukari utaisha katika kipindi hicho kutokana na Mikakati mbalimbali iliyojiwekea Bodi hiyo katika kuongeza uzalishaji wa Sukari Nchini.

Bengesi amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia suluhu hassan imedhamiria kuongeza uzalishaji wa sukari nchini kwa kujenga viwanda vingi ili kuongeza ajira kwa watanzania pia.

“Sisi kama chombo cha udhibiti chenye ufanisi na kinachoweza kuhudumia na kusaidia tasnia ya sukari kufikia ushindani na uendelevu unaotakiwa tuna jukumu la kuisaidia serikali kupunguza gharama za uagizaji wa Sukari kutoka nje na ili tufanikiwe ni lazima tuwekeze kwenye ujenzi wa viwanda,”amesema Prof.Bengesi.

Pamoja na hayo amesema kuwa watahakikisha kuwa  miradi mipya ambayo ni Kiwanda cha Sukari  Bagamoyo kimeshaanza na kwa msimu huu watazalisha tani 20,000 na mwaka 2023 wanatarajia kufikia tani 35,000 ambao ndio uwezo wa kiwanda kwa sasa.