Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online -Dodoma
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeshiriki maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma, yanayojumuisha Wizara, Sekretarieti za Mikoa na taasisi mbalimbali za umma kwa lengo la kutoa elimu kwa wadau wa ununuzi nchini na wananchi kwa ujumla.
PPAA imeshiriki maadhimisho hayo yaliyoratibiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, kwa lengo la kutoa elimu pamoja na kuonesha uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa wananchi kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na mamlaka hiyo.

Akiongea kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa PPAA, James Sando,Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Mamlaka hiyo,Nelson Kessy,amesema kupitia maadhimisho ya Wiki ya Utumishi,wametumia maadhimisho hayo imepata kutoa elimu kuhusu matumizi ya moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST.
“Pamoja na mambo mengine, moduli hii imesaidia kuokoa muda, gharama, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ununuzi wa umma na kutunza kumbukumbu kwa ujumla,” amesema Kessy.
Kessy amesema,PPAA imefanya jitihada za kuwapatia wazabuni mafunzo kuhusu matumizi ya moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST inawafikia wadau wa ununuzi wa umma ili kuisaidia Serikali kupata thamani halisi ya fedha.
Moja ya jitihada ni kutoa mafunzo kwa wazabuni na wadau wa ununuzi wa umma Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kati ambapo ilifanikiwa kutoa elimu kwa wazabuni 873,wakuu wa idara na vitengo vya ununuzi na sheria wapatao 1,588 kutoka kwenye taasisi nunuzi 500.

Awali akifungua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Utumishi, Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,George Simbachawene,amezisisitiza taasisi za Serikali kuhakikisha zinatoa kipaumbele matumizi ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi katika kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.
“Napenda kutoa wito kwa taasisi za umma zote kuhakikisha zinatumia TEHAMA vizuri ili wananchi waweze kuendelea kupata huduma bora haraka na kwa urahisi,”amesema Waziri Simbachawene.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kitaifa ni: “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidigiti ili kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na kuchagiza Uwajibikaji”.
Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika huadhimishwa kila mwaka Juni 23,na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), ikiwa ni ishara ya kutambua mchango muhimu wa watumishi wa umma katika maendeleo ya nchi zao na Bara kwa ujumla.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako