December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi yawashikilia Sungusungu waliochoma vibanda vya wavuvi, wakulima

Na George Mwigulu, Katavi

JESHI la Polisi Mkoa wa Katavi linawashililia baadhi ya Sungusungu katika Kitongoji cha Masogangwi Kata ya Itenka Halmashauri ya Nsimbo Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi kwa kuchoma zaidi ya vibanda 100 vya kuishi vya wavuvi na wakulima na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali.

Hadi sasa wanaoshikiliwa wa jeshi hilo ni Bujima Maginya (50) mkazi wa Kijiji cha Tumaini na Shalu Charles (32) mkazi wa Kijiji cha Kakese ambao bado wanaendelea kuhojiwa huku watuhumiwa wengine wakiendelea kusakwa.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga amesema kuwa tukio hilo lilitokea jana naa 8 mchana kwenye Kitongoji hicho na hadi sasa chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana.

Taarifa za awali zimedai kuwa, kabla ya tukio hilo Mtemi wa Sungusungu wa Kijiji cha Tumaini, Halawa Ligoba alifika kwenye kambi hiyo na kuwakusanya wakazi hao waliochomewa vibanda umbali wa mita takribani 100 kutokea kwenye eneo la tukio hilo .

Lengo la kuwakusanya wananchi hao ilikuwa ni kufanya nao mkutano wa hadhara na wanachi hao waliitika wito huo na waliweza kukusanyika kwenye eneo hilo na ndipo kikundi cha Sungusungu kinachoongozwa na Mtemi huyo kilifika kwenye eneo hilo huku wakiwa na silaha za jadi na kuanza kuchoma zaidi ya vibanda 100 vya makazi ya watu hao.

Amesema, baada ya kuchoma vibanda hivyo, Sungusungu hao hawakuondoka haraka mpaka hapo walipo hakikisha vibanda hivyo vya nyasi vimeteketea.

Kamanda Kuzaga amesema, Jeshi la Polisi walipata taarifa ya tukio hilo na waliweza kufika kwenye eneo hilo na waliweza kuwakamata watuhumiwa wawili ambao wanatuhumiwa kuhusika kwenye tukio hilo.