Na Penina Malundo, TimesMajira Online, Chato
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kupitia kitengo chake cha utafiti kimetoa
tathimini ya awali ya kampeni zake ambayo inaonesha kuwa kinaenda vizuri katika Mikoa mbalimbali kutokana na sera nzuri na za kisayansi anazonadi Mgombea Urais wa Chama hicho, Dkt. John Magufuli zinazogusa maisha ya wananchi hususani wa hali ya chini jambo ambalo linazidi kuwaweka kwenye nafasi nzuri ya kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 28???.
Akizungumza Wilayani Chato Mkoani Geita, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho, Humphrey Polepole amesema tathimini hiyo inaonyesha kuwa kama kura zikipigwa leo mgombea huyo ataibuka na ushindi kwa asilimia 85.
Amesema, kampeni zao zinafanyika kisayansi kwa kuzingatia weledi wa hali ya juu kwani chama hicho kimetawanya makada waandamizi na viongozi katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa lengo la kufanya kampeni kila kona.
Polepole amesema kuwa, moja ya msafara wa viongozi wanaofanya kampeni ni pamoja na msafara mkuu wa mgombea wa Urais ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha CCM, Dkt. Magufuli ambaye hadi sasa tayari ameshazunguka katika Mikoa nane ndani ya siku 10 na kukutana na maelfu ya watanzania.
“Mbali na Dkt. Magufuli ambaye ameshatembelea Mikoa ya
Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mara, Mwanza na Geita, pia yupo Mama Samia Suluhu ambaye ameshapira katika Mikoa ya Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Lindi huku Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete nae yupo Kusini akiendelea na kampeni,”.
“Pia yupo Mjumbe wa Kamati kuu wa CCM, Kassim Majaliwa kwani nae anaendelea kupiga kampeni na tayari kaenda Mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Arusha na Dodoma huku viongozi wengine wakiendelea kuwasha moto katika kampeni hii kwa kueleza wananchi mambo makubwa na mazuri ya CCM ambayo yamefanyika ndani ya miaka mitano hii,” amesema Polepole.
Mbali na viongozi hao pia, apwo wajumbe wa Kamati kuu, Mizengo Pinda na Job Ndugai ambao wao wapo Kanda ya kati wakiendelea na kampeni.
“Kampeni yetu ni ya kisayansi na tunatumia usafiri wa barabara kufika kijiji hadi kijiji,kata hadi kata,na wilaya kwa wilaya na wala hatutumii helkopta,”.
“Kampeni hii ni rahisi mno kwa sababu tunautajiri wa kazi nzuri tulizozifanya miaka mitano ya nyuma ambazo sasa tunazieleza kwa umma wa watanzania ,”
Polepole amesema, kwa miaka hiyo mitano CCM imejenga taasisi imara yenye uwezo Makada madhubuti, Wanachama wake wameimarika na idadi yao kuongezeka maradufu kwa sasa wanatafuta milioni 700 wa chama hicho.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa