May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Plan International yatoa vitabu 1,000 kwa shule 23

Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza


Shule za msingi 23 za Kata 18 za Halmashauri ya Jiji la Mwanza zimenufaika na msaada wa vitabu 1,000 vya somo la lugha ya Kiingereza vyenye thamani ya milioni 9.4, vilivyotolewa na shirika la Plan International kwa wanafunzi wa darasa la tatu na la tano.


Msaada huo ni jitihada za wadau za kupunguza uhaba wa vitabu katika shule hizo pamoja na changamoto za wanafunzi 20 kutumia kitabu kimoja hivyo kuboresha mazingira ya ufundishaji na kujifunza.


Mkuu wa kitengo cha utekelezaji wa shirika la  Plan International Tanzania Martha Lazaro,ameeleza kuwa uwepo wa vitabu vya kutosha vinavyokidhi viwango vya serikali kati ya uwiano wa kitabu na wanafunzi ni moja ya kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia pamoja na kuwa na elimu bora ambayo ni jumuishi.


Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa vitabu hivyo uliofanyika Machi 22,2024 katika shule ya msingi Mwananchi iliopo Kata ya Mahina jijini Mwanza,Lazaro ameeleza kuwa kupitia mradi wa Vijana,Elimu,Malezi na Ajira (VEMA),shirika limekuwa likifanya mambo mengi ikiwemo ya elimu ambao unafadhiliwa na shirika la Maendeleo la Ubelgiji.


“Vitabu 1,000 ni vingi lakini siyo vingi bado havitoshi kwani kuna ubaha wa vitabu 5541,vitabu hivi vitakuwa vimesaidia kwa asilimia 9.8 tu bado tuna upungufu, nawaomba wadua na serikali tuendelee kubuni njia mbalimbali ambazo zitatuwezesha kupunguza changamoto hii ili kuboresha mazingira ya elimu,”ameeleza Lazaro.

Ameeleza sababu ya kulenga nyanja ya elimu shirika linaangalia namna ya kuhakikisha watoto wanapata haki zao na kuzifurahia ili ziweze kuwafikisha kufikia ndoto zao.

“Tunatambua kupitia elimu ni rahisi mtoto kuweza kufikia zile haki nyingine kwa sababu tunaamini elimu ni ufunguo wa maisha.Mtoto anapopata elimu bora ni rahisi kupata afya bora pia kwa sababu kupitia elimu atajua nini cha kufanya magonjwa gani anaweza kuyaepuka,chakula gani anaweza kula na mfumo gani wa maisha anaopaswa kuishi ili aweze kustawi,”ameeleza Lazaro na kuongeza:

“Kupitia elimu ambayo mimi ninaiona ndiyo mlango mkuu wa haki nyingine zote,mtoto atatambua haki yake,atatambua namna ya kudai haki yake lakini pia atatambua wajibu wake na ni wapi pakupeleka malalamiko yake pale anapokutana na unyanyasaji,”.

Kwa upande wake Ofisa Taaluma Awali na Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza,Julius Magembe kwa niaba ya Ofisa Elimu Msingi wa halmashauri hiyo,ameeleza kuwa upungufu wa vitabu ni moja ya kilio kikubwa katika sekta ya elimu.


Pamoja na kilio hicho serikali inajitahidi kwa juhudi na kutumia gharama kuhakikisha vitabu vya kutosha vya shule za msingi vinapatikana.

“Vitabu hivi vinatuonesha namna ya kupambana na adui ujinga na tutamuondoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama Plan International walivyofanya leo hii,”ameeleza Magembe.

Awali Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Mwananchi Editha Alfred,ameeleza kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1625 huku akifafanua uwiano wa vitabu uliopo na idadi ya wanafunzi kwa kila darasa.


Ambapo ameeleza kuwa kwa darasa la awali wanafunzi wapo 130 uwiano kitabu kimoja wanafunzi 9,darasa la kwanza wanafunzi 236 kitabu kimoja wanafunzi 6,darasa la pili wanafunzi wapo 248 kitabu kimoja wanafunzi 3 na darasa la tatu wanafunzi wapo 205 uwiano ni kitabu kimoja wanafunzi 4.

Huku darasa la nne wapo wanafunzi 227 na uwiano ni kitabu kimoja wanafunzi 6,darasa la tano wanafunzi 187 kitabu kimoja wanafunzi 4,darasa la sita wanafunzi 181 kitabu kimoja wanafunzi 3 na darasa la 7 wanafunzi 227 kitabu kimoja wanafunzi 2.

“Serikali imeendelea kuongeza vitabu kila mwaka,tunashukuru shirika la Plan International kwa ufadhili wa vitabu,tunaamini vitapunguza uwiano mkubwa uliopo kati ya kitabu kimoja na idadi ya wanafunzi,”ameeleza Edhita.

Mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi Mwananchi Nura Chacha amelishukuru shirika hilo kwa msaada wa vitabu ambavyo vitawasaidia katika kujifunza na kuweza kufaulu somo la lugha ya Kiingereza ambalo wengi wanaona ni gumu.


Huku Mwanafunzi wa shule ya msingi Mahina Emmanuel Paul,amewaomba wadau wengine waendelee kusaidia wanafunzi kwa kuwapatia vitabu vya masomo magumu kama ya hisabati na kiingereza.