Na Jackline Martin, TimesMajira Online
NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Geofrey Pinda amewataka wadau wa msaada wa kisheria nchini kujenga na kuimarisha ushirikiano ya kimkakati na serikali ikiwa ni fursa ya kuwasilisha mapendekezo yenye tija kwa lengo la kuboresha sekta ya msaada wa kisheria nchini.
Waziri Pinda aliyasema hayo mwishoni mwa juma lililopita wakati wa kufunga kongamano la siku mbili Jijini Dodoma lililowakutanisha wadau wa sekta ya msaada wa kisheria takribani 120 kutoka Tanzania bara na visiwani kwa lengo la kutathimini utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria ya Mwaka 2017 pamoja na kuangalia huduma ya msaada wa kisheria kwa ujumla.
Alisema kuwa serikali na wadau wa sekta ya msaada wa kisheria ni wadau muhimu katika utendaji kazi hasa katika sera, sheria, masuala mbalimbali ya haki ambayo yanawahusu wananchi.
“Ninaamini kwamba ili kuwepo matunda mazuri, kunahitajika uhusiano endelevu kati ya serikali na wadau wa sekta ya msaada wa kisheria.
“Kwa kutambua hilo, nawahakikishia kuwa ofisi yangu itakuwa wazi kufanya kazi na wadau wa sekta ya msaada wa kisheria kwa kupokea taarifa, ushauri na mazungumzo mengine muhimu kuhusu mambo mbalimbali yanayowakabili wananchi katika sekta hii nyeti nchini,” alisema.
Waziri huyo aliongeza kuwa Serikali iko tayari kufanya kazi na wadau wa sekta ya msaada wa kisheria katika mazingira rafiki, huru, uwazi na usawa ili kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya msaada wa kisheria kwa kuwa lengo ni kujenga nchi moja.
Aidha, Naibu Waziri Pinda, aliwapongeza watoa huduma za msaada wa kisheria kwa kazi kubwa wanayoifanya katika jamii kwa kujitolea kwa lengo la kuwezesha jamii hususani wale wasio na uwezo wa kupata huduma za msaada wa kisheria kupata usaidizi na utatuzi wa changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo.
“Ni muhimu sisi kama Wizara ni kutathimini thamani ya utoaji wa msaada wa kisheria na kuimarisha huduma za msaada wa kisheria nchini kwa kujengea uwezo watoa huduma wa msaada wa kisheria.
“Na ndio maana sisi kama Wizara tukaona ni vyema kuondoa vikwazo kama vile ada ya mwaka kwa wasaidizi wanaojitolea bila malipo yoyote na kuendelea kuboresha huduma hizi nchini“ alisema.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala, ambao ndio waandaaji wa kongamano hilo kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, alisema kuwa kongamano hilo la siku mbili lilijadili kwa kina masuala mbalimbali na kuibuka na maazimio ambayo baadae kikosi kazi cha wadau kitaandaa ripoti na kuiwasilisha serikali kwa ajili ya utekelezaji zaidi.
“Kikao hiki kimetupa maazimio mengi. Niahidi kuwa, wataalamu wetu wamerekodi yote yaliyojadiliwa na wadau. Baada ya kongamano hili timu hiyo itaandaa taarifa rasmi kwa ajili ya kuiwasilisha serikalini ili ifanyiwe kazi kwa ajili ya kuboresha na kuongeza ufanisi wa sekta ya msaada wa kisheria nchini” alisema Ng’wanakilala.
Vilevile, Ng’wanakilala aliishukuru Serikali chini ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha inatoa mafunzo kwa watoa huduma za msaada wa kisheria na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma hizi kwa wanawake na watoto, ambao ndio wahanga wakubwa na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Akisoma hotuba fupi kuhusu masuala mbalimbali yaliyoazimiwa katika kongamano hilo, Mratibu wa Mtandao wa Watoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria nchini (TAPANET), Tolbert Mmassy, aliipongeza serikali kwa kuondoa ada ya usajili kwa watoa huduma za msaada wa kisheria, hali itakayoongeza idadi ya wadau wanaojisajili katika mfumo wa serikali na kutambulika kisheria.
Pamoja na hayo wadau wa kongamno hilo waliazimia mambo mbalimbali ambayo yanahitaji kuboresha sekta ya msaada wa kisheria ikiwemo; kutambulika kwa wasaidizi wa kisheria kila ngazi ili waweze kuwahudumia wananchi, watoa huduma za msaada wa kisheria kupewa ofisi katika majengo ya umma ili kuwasaidia watu wengi zaidi wenye uhitaji, utekelezaji wa shughuli za huduma za msaada wa kisheria kwa kushirikiana na serikali ili kuongeza wigo wa huduma za msaada wa kisheria kwa wadau mbalimbali,watoa huduma za msaada wa kisheria kujengewa uwezo kwenye mifumo na sheria jinai pamoja na kuiomba serikali kutenga ruzuku maalumu katika kutoa msaada wa kisheria ili kuhakikisha kuwa huduma hizi zinakuwa endelevu.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa