January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PAC yaitaka MWAUWASA kutoa elimu utunzaji mazingira,yaridhishwa ufanisi wa mradi

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeitaka Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Mwanza(MWAUWASA) kuelimisha wananchi umuhimu wa kutunza mazingira pamoja na kutovamia vyanzo vya maji kwa ustawi wa uhai wa binadamu.

Pia Kamati hiyo imeridhishwa na ufanisi wa mtambo wa kuzalisha na kutibu maji mradi wa chanzo cha maji Butimba mkoani Mwanza huku ikipongeza jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kufanikisha mradi huo.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Japhet Hasunga akibonyeza kitufe kwenye Laptop ikiwa ni kiashiria cha kuwasha maji yaliopo katika mabwawa ya cha kipya cha maji Butimba Machi 23, 2024 ,ambapo kamati hiyo ilitembelelea na kukagua shughuli ya uzalishaji maji inayoendelea sambamba na hatua mbalimbali za ukamilishwaji wa mradi huo uliopo wilayani Nyamagana mkoani Mwanza

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Japhet Hasunga,ameeleza kuwa wao wanataka mradi unapojengwa kama hivi suala la mazingira lipewe uzito unaostahili ikiwa ni pamoja na upandaji wa miti,utunzaji wa mandhari ya maeneo haya na wananchi waelimishwe wasivamie katika maeneo ya vyanzo vya maji kwa sababu wakifanya hivyo maana yake maisha ya binadamu yatakuwa hatarini.

Hasunga amesema hayo Machi 23, 2024 mara baada ya kamati hiyo kutembelelea na kukagua shughuli ya uzalishaji maji inayoendelea sambamba na hatua mbalimbali za ukamilishwaji wa mradi wa chanzo cha maji wa Butimba.

“Katika maeneo mengi kumekuwa na changamoto,tunajua mazingira ndio uhai wetu na maisha yetu ya nategemea hicho lakini unakuta miradi kama hii ambayo serikali inawekeza fedha nyingi baadae watu wanaharibu mazingira na kusababisha miradi inabaki bila kuweza kukidhi mahitaji au matarajio tulikuwa nayo,tunawapongeza MWAUWASA kwenye eneo hili mmeweka uzio ambao utasaidia kupunguza uvamizi lakini bado mnatakiwa kupanua zaidi na wananchi waelimishwe umuhimu wa utunzaji wa mazingira,”ameeleza Hasunga na kuongeza;

“Kwa tulichokiona kinavutia na kinafurahisha, tumeanzia pale maji yanapochotwa ziwani hadi hatua ya mwisho ambapo maji safi na salama yanaruhusiwa kufika kwa wananchi, tulichokiona kwa macho ni kitu kizur, ni mradi mzuri,”.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA),Hellen Bogohe amesema mradi huo ni wa kipekee kuwahi kujengwa nchini na mpaka kufikia Juni mwaka huu maeneo yote yatapata maji ambayo yanastahili kupata kupitia chanzo cha Butimba.

“Ni kweli mradi unavutia kama mlivyosema, changamoto zilikuwa nyingi lakini kwa umahiri wa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha nyingi ili kupunguza adha kwa wananchi, tuanaahidi kupitia mipango tunayoendelea nayo huduma itakuwa imesambaa maeneo mengi zaidi,”amesisitiza Bogohe.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Neli Msuya ameelezea kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na uzalishaji unafanyika kulingana na usambazaji unavyokwenda na kwamba hatua zinazoendelea ni za kuboresha mifumo ya usambazaji maji ili kufikia wananchi wengi zaidi kadri ambavyo mradi ulivyotarajiwa kufika.

“Chanzo kimekamilika na kazi inayofanyika sasa ni ya kulaza mabomba ya kusambaza maji,ipo mikakati ya kuweza kuboresha huduma za maji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu mikuu ya kusambaza maji kwa maana ya kuongeza mtandao wa bomba, kujenga matenki ya kuhifadhi maji ili maji kufikia wananchi wengi na hasa waishio milimani,” amesema.

Amesema ili kufikisha huduma ya maji kwa uwiano katika maeneo tarajiwa, mradi wa ujenzi wa matenki unakwenda kuanza hivi karibuni huku MWAUWASA inatarajia kukarabati na kupanua ntambo wa kuzalisha maji wa Capripoint.

Maeneo yatakayokuwa na matenki yatakayopokea maji haya ya Butimba ni Kisesa lita milioni 5,Nyamazobe lita milioni 5, Buhongwa lita milioni 10, Fumagila ya Juu (Kishiri) lita milioni 10 na Usagara lita milioni 1.

Hata hivyo Mbunge wa Jimbo la Magu Boniventure Kiswaga, ameeleza kuwa mradi huu ulipofikia kwa wao wanatarajia kupata maji ikiwemo Magu kwa eneo la Kisesa na Bujora wanayo matumaini kwamba sasa wananchi wao wanaenda kupata maji safi na salama.

“Kwangu Magu kupitia mradi huu sasa hivi wanajenga tenki la maji lenye ujazo wa lita milioni 5,ambalo litatosheleza Mji Bujora na Kisesa ambao una watu zaidi ya 100,000 na kwa sasa tunapata maji kidogo kupitia mradi wa matokeo ya haraka,”.

Nao baadhi ya wananchi wa jijini Mwanza akiwemo Eliza Gipson mkazi wa Sawa ya chini ameeleza kuwa kwa miaka hii mitatu wamepata ukombozi wa maji kwani miaka ya nyuma walikuwa wanateseka kwa kufuata maji kwa umbali mrefu.