April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mavunde akabidhi leseni 19 wachimbaji wa dhahabu

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Songwe.

WAZIRI wa Madini, Anthon Mavunde, amesisitiza kuwa ataendelea kufuta leseni kwa wamiliki wote ambao wanakiuka taratibu, lengo likiwa ni kuondoa kabisa ujanja ujanja kwenye sekta ya madini hapa nchini.

Mavunde ametoa angalizo hilo, ikiwa ni siku chache baada ya kutangaza kufuta maombi na leseni za utafiti 2648 ili kupisha waombaji wengine kupata fursa ya kuomba na kuyaendeleza  maeneo hayo kwa manufaa ya taifa na ukuaji wa sekta ya madini.

Ametoa kauli hiyo, Machi 24, 2024, kwenye mkutano wa hadhara wa wachimbaji wadogo na wananchi wa kata ya Saza, Wilayani Songwe, ambapo pia alikabidhi leseni ndogo 19 kwa wachimbaji wa kikundi cha Songwe Gold Family (SGF) .

Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, leseni hizo 19 zilizokabidhiwa kwa wachimbaji hao wadogo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan la kutaka wachimbaji hao kupatiwa maeneo ya kuchimba baada ya kuwepo malalamiko ya muda mrefu ya kutaka wapatiwe maeneo katika eneo la mlima Elizabeth lililopo katika kata hiyo ya Saza.

“Mbunge wa Songwe,Philipo Mlugo kwa kushirikiana na uongozi wa Halmashauri mna deni kubwa,kwani kilio chenu Mheshimiwa rais amekisikia na leo nimefika hapa baada ya Rais kunielekeza nije kuwakabidhi leseni zenu mlizomuomba, kwa kuwa mnaenda kuwekeza mitaji yenu kwenye maeneo yenye uhakika tunatarajia mtaongeza mzunguko wa fedha zitokanazo na shughuli za madini ili wilaya hii nayo iwe mchangiaji mkubwa wa mapato katika serikali” alisema Mavunde.

Mavunde alisema leseni hizo ndogo 19 zimetoka kwenye leseni hodhi ya utafiti  namba 9, ikiwa ni miongoni mwa leseni nyingine tatu ambazo ni namba 10, 121 na 12 ambazo zilikuwa zikimilikiwa na kampuni ya Bafex Tanzania limited na baadae kurejeshwa serikalini.

Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa kikundi cha Songwe Gold Family (SGF), Simon Ndaki, aliishukuru serikali na kusema kuwa wachimbaji wadogo katika wilaya ya Songwe kwa muda mrefu wamekuwa wakisumbuka kupata maeneo ya uchimbaji na baada ya yao wamepoteza mitaji kutokana na kwenda kuwekeza na kuchimba kwa kubahatisha.

Akizungumza katika mkutano huo, mbunge wa Songwe, Mulugo aliishukuru serikali kwa kutatua changamoto hiyo iliyodumu kwa muda mrefu.

Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Itunda ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa , Danel Chongolo, alisema kuwa asilimia 70 ya mapato ya Wilaya hiyo yanatokana na shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ametoa siku 14 kwa Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Solomon Itunda, kuhakikisha kwamba eneo la leseni tatu ambazo ni namba 10, 11 na 12 linakuwa wazi kwani wiki hii serikali inatarajia kutangaza zabuni kwa ajili ya wachimbaji wakubwa.