May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ongezeko la watu chanzo cha magugu maji kwenye bwawa la Mabayani

Na Hadija Bagasha TimesMajira Online, Tanga

Ongezeko la watu linaloambatana na shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji vya mto Zigi limetajwa kuwa chanzo cha magugu maji kwenye bwawa la Mabayani na kusababisha asilimia 30 ya bwawa hilo kuliwa magugu maji jambo ambalo linahatarisha ustawi wa bwawa hilo.

Hayo yamesemwa na Afisa wa kanda ya Muheza kutoka Tanga Uwasa Ramadhani Nyambuka wakati wa ziara ya mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Tanga katika vyanzo vya maji vinavyosimamiwa na mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira Tanga (Tanga Uwasa).

Lengo la ziara hiyo ya siku moja ni kukagua vyanzo vya maji na kuona shughuli za uhifadhi wa vyanzo zinazofanywa na Tanga Uwasa kwa kushirikiana na UWAMAKIZI katika vijiji vilivyopo kando kando ya mto zigi na bwawa la Mabayani.

Akizungumza katika ziara hiyo Nyammbuka amesema ongezeko hilo la shughuli za kibinadamu bado ni tatizo kwani wananchi wanaoishi kandokando ya bwawa hilo wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa kuleta madhara kwenye bwawa ikiwemo ongezeko la tope kwenye maji.

“Ongezeko la shughuli za kibinadamu sehemu ya juu ya mto zigi zimeongezeka shughuli zao zinategemeana na mto sasa wale wananchi kule wanachangia sana kuleta madhara kwenye bwawa na miongoni mwa madhara hayo ni kuongezeka tope katika bwawa linalisababusha kina cha bwawa kipungue, “

Aliongeza kuwa ukiondoa hilo usafi wa maji pia unapungua na kusababisha mimea kukua kwa wingi katika bwawa na hatimaye inaongeza magugu maji katika bwawa karibu asilimia 30 ya bwawa limeliwa na magugu maji.

Nyambuka alisema hapo awali waliunda kamati ya mazingira ambayo ilionyesha kufanya vizuri na watu waliheshimu na kuacha kuchoma misitu , hakukuwa na ukataji wa miti ovyo sababu kamati hizo zilikuwa zinatoka kijijini hapo.

“Bado kuna tatizo kuna watu wanafuga maeneo ya jirani na bwawa hili, wana vyoo karibu lakini pia wana shughuli za kibinadamu na zile zote zinatiririsha na kuleta mtoni na hivyo kuongeza nitrate zile zote zinakuza majani kwenye bwawa na matokeo yake magugu maji yameongezeka sana na bwawa limepungua ule ukubwa wake uliokuwepo.

Awali mkuu wa wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa amesema kuwa kitendo cha shughuli za kibinadamu kuendelea kufanyika katika vyanzo vya maji ni jambo ambalo kamati ya usalama haiwezi kulivumilia hivyo hatua za makusudi za haraka zitachukuliwa ikiwemo kuimarisha ulinzi katika eneo hilo wakati wote.

Alisema moja ya wajibu wao ni kuhakikisha bwawa hilo linaendelea kubaki salama na linaendelea kuhifadhi maji lakini pia kuhakikisha eneo hilo linakuwa safi wakati wote.

“Niwakumbushe kuwa ni wajibu wangu ni kuendelea kulisimamia hilo kwamba watu wanaofanya shughuli kandokando ya vyanzo vya maji tunaendelea kuwaondoa iwe kwa hiari, kwa kuwaomba au kwa lazima wana kila sababu ya kuendelea kupisha ili tuendelee kupata zawadi hii ambayo Mwenyezi Mungu katujaalia katika miaka yote, “amesisitiza DC Mgandilwa.

Hata hivyo Mgandilwa amewataka viongozi wa kata na mitaa hususani wanaosimamia mazingira kuendelea kuhamasisha wananchi kuachana na biashara ya matumizi ya mkaa na badala yake waone namna wanaweza kutumia nishati nyingine rafiki kwa mazingira ikiwemo gesi ili kuepusha ukataji wa miti hovyo na hatimaye kusababisha uharibifu wa mazingira.

Kwa upande meneja ufundi Tanga Uwasa mhandisi Rashidi Shabani ameipongeza serikali kwa kuungana nao ili kutekeleza jitihada za uhifadhi wa vyanzo vya maji ili maji yawe endelevu katika Mkoa wa Tanga.

Mhandisi Rashid amewaomba wananchi walioko kando kando ya mto zigi na bwawa la mabayani kuendelea kushirikiana nao katika kutunza mazingira ikiwemo kupanda miti ili kutengeneza uoto utakaochochea mvua kuwepo na utakaochochea uwepo wa maji safi na salama.