November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ongezeko la matumizi ya tumbaku kwa wanawake yanavyoweza kuathiri watoto

Na  Aveline Kitomary,TimesMajira Online,Dar es Salaam

KILA ifikapoi 31 Duniani huadhimisha siku ya kutotumia tumbaku ambapo lengo ni kutoa elimu kuhusu madhara ya matumizi ya tumbaku.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Kutotumia Tumbaku Duniani kwa mwaka 2021 ni “Dhamiria kuacha kutumia tumbaku na bidhaa zake”.

 Kaulimbiu hii inalenga kuhamasisha jamii kuacha matumizi ya tumbaku kwa kuelimisha jamii kuhusu madhara ya kiafya ya tumbaku na bidhaa zake na uhusiano uliopo kati ya matumizi ya tumbaku na magonjwa yasiyoambukiza (NCD).

 Vilevile, Kaulimbiu hiyo inahimiza kuwepo kwa mipango na hatua za Serikali na jamii za kupunguza visababishi vya magonjwa yasiyoambukiza kutokana na tumbaku.

Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali huadhimisha siku hiyo kwa kuelimisha Dunia kuhusu madhara ya kiafya yatokanayo na matumizi ya bidhaa za tumbaku kwa njia mbalimbali ikiwemo kuvuta, kunusa au kutafuna.

 Baadhi ya madhara ni pamoja na kuongeza uhatarishi wa kutokea kwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya saratani, magonjwa ya njia ya hewa, mapafu, kisukari ,moyo, mishipa ya damu na kuongeza uhatarishi wa shinikizo la juu la damu.

 Tumbaku hupunguza kiwango cha oksijeni inayoweza kusafirishwa na damu na hivyo kuwa na uwezekano wa kuifanya damu kuganda jambo linaloweza kusababisha magonjwa mengine ya moyo, ambayo nayo huweza kusababisha kiharusi au kifo cha ghafla.

 HALI ILIVYO

Kwa mujibu wa Wizara ya afya  takribani watu milioni 6 hufariki kutokana na matumizi ya tumbaku au kukaa karibu na mvutaji, ambayo huchangia asilimia 6 ya vifo vya wanawake na asilimia 12 vya wanaume kwa mwaka.

Inakadiriwa kuwa  ifikapo mwaka 2030 vifo vitokanavyo na matumizi ya tumbaku vitaongezeka na kufikia zaidi ya milioni 8 kwa mwaka.

Hata hivyo, mtu anaweza kuepuka matumizi ya tumbaku na hivyo kuwa na dunia ya watu wasiotumia tumbaku kabisa.

Aidha, kila mwaka watu 600,000 hufariki kutokana na kuvuta moshi wa wavutaji kwa kuwa karibu na wavutaji ambapo kati yao asilimia 28 ni watoto.

TAFITI ZILIZOFANYIKA

Tafiti za viashiria hatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza (Steps Survey) ya mwaka 2012 ilifanywa na  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO).

 Utafiti huu ulionesha kuwa, wastani wa asilimia 14 ya watanzania wanatumia tumbaku ambapo wanaume ni asilimia  26 na wanawake ni asilimia 2.9.

Ripoti hii pia inaonesha kuwa kuna idadi kubwa ya watu wanaoathirika kwa moshi wa tumbaku toka kwa wavutaji ambapo asilimia 17.5 huathiriwa na wanaovuta sigara majumbani na asilimia 24.9 sehemu za kazi.

Aidha, utafiti mwingine ni uchunguzi wa matumizi ya tumbaku wa watu wazima (Global Adult Tobacco Survey) uliofanyika nchini Tanzania mwaka 2018 ambao ulionesha kuwa asilimia 8.7 ya watu wazima wanavuta tumbaku na bidhaa zake ambayo ni sawa na watu wazima milioni 2.6 huku kati yao asilimia 14.6 wakiwa ni wanaume na asilimia 3.2 ni wanawake.

Taarifa hii inaonesha mafanikio kwenye kupunguza matumizi ya tumbaku kwa ujumla na hasa kwa wanaume, ingawa kumekuwa na ongezeko la matumizi ya tumbaku kwa wanawake ukilinganisha na takwimu za mwaka 2012.

Aidha, utafiti huo pia ulionesha asilimia 32.9 ya watu wazima walionekana kuvuta moshi wa watumiaji wakiwa wanafanya shughuli kwenye maeneo ya ndani ambao walikuwa sawa na watu wazima milioni moja.

Asilimia 13.8 ya watu wazima sawa na watu wazima milioni 4.1 wakiwa maeneo ya majumbani, asilimia 31.1 ya watu wazima sawa na watu milioni 3.5 wakiwa kwenye maeneo ya migahawa, na asilimia 77 sawa na watu wazima milioni 3 wakiwa maeneo ya baa na kumbi za starehe za usiku.

Taarifa nyingine ni ya uchunguzi wa hali ya matumizi ya tumbaku kwa vijana (Global Youth Tobacco Survey) wa mwaka 2008 uliofanyika nchini Tanzania ambapo ilibainika kuwa uwiano wa vijana waliowahi kutumia tumbaku ya aina yoyote ile katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ilikuwa asilimia 9.7.

MADHARA KWA WATOTO

Tafiti zilizofanyika zinaonesha kunaongezeko la wanawake wanaotumia tumbaku na bidhaa zake.

Lakini Je jamii inaulewa wowote kuhusu namna mama mjanzito anavyoweza kuathiri maisha ya mtoto akiwa tumboni na baada ya kuzaliwa?

Daktari  Bingwa wa Watoto kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili(MUHAS)  Fransis Furia anasema  madhara makubwa  kwa mtoto aliyeko tumboni endapo mama mjamzito atatumia tumbaku au kukaa karibu na watu wanaotumia bidhaa hizo ni pamoja na kupata ugonjwa hatari wa saratani.

Anaeleza kuwa  madhara yanayotokea ni mtoto kuzaliwa akiwa njiti  na pia kuna uwezekano mkubwa wa mimba kuharibika.

“Naweza kusema kuwa hata mimi  navuta sigara kwasababu sio lazima uvute moja kwa moja ila ukikaa na mtu anayevuta na wewe pia unavuta katika uvutaji sigara sio mtu mmoja tu anaathirika lakini pia wale watu ambao wako karibu na mvutaji.

“Hayo matatizo pia yanaweza kumuathiri mama mjamzito akivuta sigara au kukaa na watu wanaovuta sigara  inaleta madhara kwa mtoto  kwani huathiri ukuaji na mama kupata shinikizo la damu hali ambayo inaweza kusababisha mimba kuharibika,”anabainisha Dk Furia.

 Anaongeza “Tumeshasikia akinamama wakipoteza maisha na nilishawahi kupata kesi ya mama mmoja mimba ilitoka mara saba lakini yeye hatumii kwasababu tu anakaa na mtu anayetumia.

mkulima akivuna Zao la tumbaku

“Tafiti zinaonesha kuwa mtoto akizaliwa njiti wakati wa ukubwani anaweza kupata magonjwa yasiyo ya kuambukizwa baadae kama matatizo ya  figo,kisukari,shinikizo la damu pia anaweza kupata shida ya kifua kama pumu .

“Mtoto  anayekaa nyumbani na baba yake yanavuta sigara inamaana mfano mpaka anamaliza kidato cha nne amevuta sigara kwa miaka 14.

HATUA ZINAZOCHUKULIWA

 Waziri wa Afya Maendoleo ya Jamii,Jinsi ,Wazee na Watoto,Dk Doroth Gwajima,  anasema serikali inaenelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo Kuongeza uelewa kwenye kundi kubwa la jamii juu madhara yanayoweza kupatikana kutokana na kutumia tumbaku au kuwa karibu na mtu anayetumia tumbaku.

“Kuwapa moyo na  kuongeza nguvu kwenye utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa kudhibiti matumizi ya bidhaa za tumbaku.

 “Serikali inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, ambayo inalenga kutoa huduma kwa magonjwa yasiyoambukiza kwa umahiri zaidi.

“Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kudhibiti matumizi ya bidhaa za tumbaku  ikiwemo kuridhia mkataba wa Kimataifa wa kudhibiti matumizi ya bidhaa ya tumbaku na kuwa kati ya nchi 168 zilizoridhia mkataba huo na hivyo nchi yetu kutengeneza Sheria ya Tumbaku ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za Mwaka 2004 ,”anaeleza Dk Gwajima.

Anabainisha kuwa serikali inapiga marufuku uvutaji wa sigara na bidhaa zake kwenye maeneo ya wazi na kutoa elimu kwenye majukwaa mbalimbali kuhusu madhara ya tumbaku.

Anaeleza kuwa Serikali pia inaendelea kusisitiza kuacha utumiaji wa aina ya bidhaa ya tumbaku iitwayo Shisha.

“Udhibiti wa tumbaku pia umeanishwa katika Ajenda ya Maendeleo Endelevu kwa vile unatambulika kama mkakati madhubuti wa kusaidia kufanikisha lengo namba 3.4 la Malengo ya Maendeleo Endelevu la kupunguza theluthi ya vifo vya mapema duniani kote, vinavyosababishwa na magonjwa yasiyoambukiza.

“Ikiwemo magonjwa ya moyo, saratani na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa ifikapo mwaka 2030.

 “Kutekeleza Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Matumizi ya Tumbaku, ni lengo lingine la ziada ambalo litaoanishwa na mipango ya Serikali pamoja na jitihada hizi, bado nguvu zaidi inahitajika ili kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi na kuhamasika, bila kushurutishwa kuacha kutumia tumbaku kwa faida yao na nchi kwa ujumla,”anafafanua.

Anasema kuwa gharama za kuwatibu wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza kutokana na matumizi ya tumbaku, zinaathiri maendeleo ya nchi na familia kwani fedha hizo zingetumika kwa mambo mengi ya maendeleo.

 “Ikumbukwe kuwa Serikali peke yake bila wadau haiwezi kufikia malengo yaliyowekwa ili kudhibiti matumizi ya tumbaku.

“Wavutaji wanaweza kuacha kuvuta, au kutafuta msaada kusaidiwa ili kulinda afya zao na za wanaowazunguka ikiwemo watoto, wanafamilia na marafiki,Pia pesa inaweza kutumika kwa vitu vya msingi, kama ununuzi wa chakula bora, matibabu na elimu.

“Wito kwa kila mmoja wetu kushiriki kikamilifu katika kuelimisha jamii nzima kuhusu madhara yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku na umuhimu wa kujilinda dhidi ya moshi wa tumbaku hususani kwa wale wasiotumia tumbaku.

“Nitoe rai kwa vijana watambue kuwa, tumbaku ina madhara mengi ya kiafya na hivyo wajitahidi kuepukana na matumizi ya bidhaa za tumbaku, maana wao ndio taifa la leo na kesho,”anashauri Dk Gwajima.