September 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ONE GIRL PLUS yazinduliwa kuwafikia Watoto wa Kike 

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

SERIKALI imewataka wadau wa maendeleo nchini, wakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali, kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwawezesha watoto wa kike kushiriki kikamilifu katika masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

Kauli hiyo ilitolewa juzi jijini Dar es Salaam na Mwakilishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Felister Mapunda, wakati wa uzinduzi wa mfumo wa kidijitali wa One Girl Plus unaotekelezwa na Msichana Initiative.

Amesema Serikali kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo pamoja na mtaala ulioboreshwa, imeendelea kusisitiza matumizi ya sayansi na teknolojia katika elimu ili kuwaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya sasa ya jamii na soko la ajira.

“Unapomuelimisha msichana haumsaidii peke yake, unawezesha familia, unaimarisha jamii na unawekeza katika kizazi kijacho,” amesema.

Mapunda amesema msichana mwenye ujuzi ana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, kujilinda, kujiamini, kujenga maisha yake na kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii.

Amesema mfumo wa One Girl Plus unaweza kuwa daraja kati ya msichana na fursa, kati ya ndoto na utekelezaji, pamoja na kati ya changamoto za leo na Tanzania inayotarajiwa kesho.

Aidha, amesema Wizara ya Elimu imekuwa ikishirikiana na Msichana Initiative katika kuhakikisha wasichana wanapata haki ya elimu na mazingira yanayowawezesha kuishi kwa heshima na kufikia ndoto zao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Msichana Initiative, Consolata Chikoti, amesema pamoja na wasichana kupata elimu shuleni, bado kuna umuhimu wa kuwajengea stadi za maisha zinazowasaidia kujitambua, kujiamini na kuweka malengo.

Amesema hali hiyo imeifanya taasisi hiyo kutumia teknolojia kama njia ya kuwafikia wasichana wengi zaidi.

“Tumeona kwamba ijapokuwa wasichana wanapata elimu mashuleni, kuna pengo kubwa katika kupata stadi za maisha zinazowafundisha kujitambua, kujiamini na kujiwekea malengo,” amesema.

Chikoti amesema One Girl Plus imejengwa ili kuwasaidia wasichana kukuza kujiamini, kupata stadi za maisha na kuwa na uwezo wa kuweka malengo ya maisha yao.

Naye Mkuu wa Mawasiliano wa Msichana Initiative, Sara Bedah, amesema programu hiyo ilianza miaka minne iliyopita kwa kutumia mikutano ya ana kwa ana shuleni na hadi sasa imewafikia zaidi ya wasichana 10,000.

Amesema kuanzishwa kwa mfumo wa kidijitali kutasaidia kuongeza wigo wa programu hiyo na kuwafikia wasichana wengi zaidi katika maeneo mbalimbali.