Na Joyce Kasiki, Geita

USHIRIKIANO na wawekezaji kutoka China umemwezesha mchimbaji aliyekuwa katika mchakato wa kufuta leseni zake kurejea katika shughuli za uchimbaji baada ya kukabiliwa kwa muda mrefu na ukosefu wa mtaji, teknolojia na changamoto ya maji kujaa katika maduara ya madini.
Akizungumza kuhusu safari hiyo, Emmanuel Jirab kutoka Kampuni ya Yi Xing Kuangye Mining Co. Ltd amesema mchimbaji huyo alikuwa ameshindwa kuendeleza shughuli zake kutokana na changamoto hizo, hali iliyosababisha leseni zake kutotumika kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Jirab, kutokana na kukosa uwezo wa kifedha na vifaa vya kukabiliana na maji yaliyokuwa yakijaa katika maeneo ya uchimbaji, mchimbaji huyo alianza kuona leseni zake kama mzigo na kuamua kuandika barua kwenda Wizara ya Madini akiomba zifutwe rasmi.
Hata hivyo, wakati akisubiri mchakato wa maombi hayo, wawekezaji kutoka China walifika kwake bila yeye kuwatafuta, wakatembelea maeneo yake ya uchimbaji na kuonyesha nia ya kushirikiana naye katika kuendeleza shughuli hizo.
“Wawekezaji walipokuja, walikuja wenyewe nyumbani, mimi sikuwatafuta. Wakatembelea na kukubali kwamba tutafanya nao uchimbaji,” amesema Jirab.
Baada ya kufikia makubaliano ya ushirikiano, mchimbaji huyo alirejea Wizara ya Madini kuzuia mchakato wa kufuta leseni zake, hivyo kuziwezesha kuendelea kuwa hai kwa ajili ya shughuli za uchimbaji.
Jirab amesema kupitia ushirikiano huo, shughuli za uchimbaji zilianza tena katika maeneo yaliyokuwa yamesimama kutokana na ukosefu wa mtaji na changamoto ya maji.
Amesema kurejea kwa shughuli hizo kumemwezesha mchimbaji huyo kuanza kupata mafanikio ya kifedha na kugharamia mahitaji mbalimbali ya familia yake, ikiwemo elimu ya mtoto wake anayesoma nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Jirab, hali hiyo inaonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya wachimbaji na wawekezaji, hasa pale wachimbaji wanapokabiliwa na changamoto za mtaji, teknolojia na vifaa vya kisasa.
Mchimbaji huyo pia ameishukuru Serikali na Wizara ya Madini kwa fursa na mazingira wezeshi yaliyomsaidia kuendelea kunufaika na rasilimali za madini nchini.

More Stories
C-CEOs Forum kuwa chachu utekelezaji Dira 2050
Wadau waongeza mikakati kuimarisha Elimu Nchini
Range ang’ara riadha BAMATA