September 27, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mnyeti: Maonesho ya Madini yaonyesha Teknolojia mpya


Na Joyce Kasiki, Geita


MKUU wa Mkoa wa Geita, Alexander Mnyeti, amesema Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini Geita 2026 yanatoa fursa kwa wachimbaji, wazalishaji, wasambazaji wa teknolojia, wawekezaji na taasisi mbalimbali kukutana na kubadilishana uzoefu kuhusu matumizi sahihi ya teknolojia katika sekta ya madini.


Akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mnyeti amesema maonesho hayo, yaliyoanza Septemba 23 na yanayoendelea hadi Oktoba 3, 2026, yanalenga kukuza matumizi ya teknolojia katika kuongeza uzalishaji na mchango wa madini katika pato la Taifa.


Maonesho hayo yanafanyika chini ya kaulimbiu, “Madini ni Utajiri, Tuwajibike kwa Pamoja Kufikia Dira ya Taifa 2050.”


Mnyeti amesema moja ya malengo ya maonesho hayo ni kuyawezesha kuwa miongoni mwa maonesho bora ya teknolojia ya madini na sekta zinazohusiana na madini barani Afrika ifikapo mwaka 2035.


Amesema pia maonesho hayo yanaunganisha wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa teknolojia na wachimbaji, wachenjuaji na wafanyabiashara wa madini, ili kuwezesha upatikanaji wa teknolojia zinazoweza kuongeza tija katika shughuli zao.


Aidha, amesema maonesho hayo yanatoa nafasi kwa wachimbaji kuwasiliana na taasisi za Serikali, wizara, wadau wa madini na taasisi zinazohusika na udhibiti na uhifadhi wa mazingira.


Kwa mujibu wa Mnyeti, maonesho hayo pia yamewakutanisha wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo katika mnyororo wa thamani wa madini kwa ajili ya kujadili na kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili.


Jumla ya washiriki 765 wanatarajiwa kushiriki katika maonesho hayo, wakiwamo wawakilishi wa kampuni za uchimbaji, taasisi za umma, wajasiriamali, wachimbaji wadogo, taasisi za fedha, kampuni zinazouza vifaa vya uchimbaji na utafiti pamoja na watoa huduma mbalimbali.


Mnyeti amewashukuru wadau mbalimbali kwa udhamini na michango yao iliyowezesha maandalizi na utekelezaji wa maonesho hayo.


Amesema ushiriki wa wadau kutoka sekta mbalimbali ni muhimu katika kuimarisha mnyororo wa thamani wa madini na kuhakikisha teknolojia inatumika ipasavyo kuongeza tija na manufaa ya sekta hiyo kwa Taifa.