December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ole Sanare aahidi neema upande wa ngumi

Na Halfan Diyu, Morogoro

UONGOZI wa Mkoa wa Morogoro umesema utaendelea kuweka mazingira mazuri na kuimarisha shughuli za michezo mbalimbali ikiwemo wa ngumi baada ya mabondia kutoka Mkoa huo kufanya vizuri katika mapambano mbalimbali waliyocheza hivi karibuni.

Ahadi hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare katika hafla fupi ya kumpongeza bingwa wa Taifa Twaha Kassim ‘Kiduku’ baada ya kumpiga kwa pointi mpinzani wake Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ na kumaliza ubishi uliodumu kwa miaka mingi.

Amesema, serikali ya Mkoa huo itahakikisha inazidi kudumisha michezo mbalimbali kwa kuwashirikisha wadau wa michezo husika ili kuendelea kuwapa fursa vijana ya kushiriki michezo na kujipatia kipato.

Ole Sanare amesema kuwa, kitendo cha kuchukua ubingwa wa Taifa ambacho kimefanywa na Kiduku kinapaswa kuungwa mkono na wana Morogoro wote na wapenda michezo kote nchini kwa kuwa bondia huyo ameuletea sifa Mkoa na kuutangaza mchezo wa ngumi ndani na nje ya nchi.

“Ulichokifanya Kiduku ni heshima kwako, kwa mchezo wa ngumi na kwa Mkoa wa Morogoro, hivyo unastahili pongezi kubwa kwa kazi ngumu uliyofanya ya kuchukua ubingwa kwani wote tunafahamu mchezo huu unatakiwa uwe na nguvu na utumie akili pia ili kuweza kushinda” amesema kiongozi huyo.

Katibu Tawala Mkoa, Mhandisi Emanuel Kalobelo amesema kuwa, Mkoa huo una historia ndefu katika mchezo wa ngumi huku ukiwa umeshawahi kutoa mabondia mahiri kama Titus Simba ambaye alifanikiwa kunyakua medali ya fedha katika mashindano ya Jumuiya ya Madola mwaka 1980 huko Scotland nchini Uingereza .

Amesema, alichofanya Kiduku ni muendelezo wa kuonesha mabondia kutoka Morogoro walivyokuwa na uwezo wa kufanya vema katika mchezo wa ngumi, hivyo serikali ya Mkoa itaendela kuwasapoti katika changamoto mbalimbali watakazokuwa wakikabiliana nazo.

Kwa upande wake, Kiduku amesema kuwa, amefarijika sana na pongezi hizo na hakuwahi kuwaza hata siku moja kuna siku atakuja kusimama mbele ya viongozi wote wa Mkoa na kumpongeza kutokana na kazi anayofanya ya kucheza mchezo wa ngumi.

Amesema, kutokana na heshima waliyomuonesha, atahakikisha anazidi kuupa heshima zaidi mkoa wa Morogoro, kwa kushinda mapambano mbalimbali yaliyopo mbele yake huku akiwaalika viongozi hao kuja kushuhudia pambano lake la Oktoba 30 dhidi ya bondia kutoka nje ambalo litafanyika jijini Dar es Salaam.