Na Joyce Kasiki, Tanga
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema Tanzania imejipanga kuhakikisha vijana wenye ujuzi wanapata fursa ya kushiriki mashindano ya kitaifa, Afrika na kimataifa ili kuonesha uwezo wao katika taaluma mbalimbali.
Profesa Nombo aliyasema hayo lwo Agoati 19 2026 alipotembelea banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), kwenye maonyesho ya Kitaifa ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu yanayoenda sambamba shindano la ujuzi (Worldskills ) ambapo alishuhudia vijana wakionesha ujuzi wao katika mashindano ya kitaaluma yanayolenga kupata wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
Amesema mashindano hayo ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuwajengea vijana uwezo wa vitendo, sambamba na elimu wanayoipata darasani, kwa kuwapeleka katika mazingira halisi ya kazi, viwandani na maeneo mengine ya uzalishaji.
“Tunataka vijana waende kwenye maeneo halisi ya kazi ili wapate ujuzi unaohitajika, badala ya kutegemea ufundishaji wa darasani pekee,” amesema Profesa Nombo.
Amesema Tanzania, ambayo sasa ni mwanachama wa mashindano ya WorldSkills, imeanza kuandaa vijana kwa kuzingatia vigezo vya kimataifa, ambapo washindi wa ngazi za chini huchaguliwa kushiriki ngazi za kitaifa na baadaye Afrika na kimataifa.
Kwa mujibu wa Profesa Nombo, vijana wanaoshiriki mashindano hayo watafanyiwa tathmini na wataalamu ili kubaini watakaoiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Afrika yanayotarajiwa kufanyika nchini Algeria mwaka huu.
Amesema Serikali pia imeanza kushirikiana na wataalamu wa mashindano ya kimataifa ili kujifunza mifumo na viwango vinavyotumika katika mashindano hayo, hatua inayolenga kuwaandaa vijana kushindana kwa kujiamini katika jukwaa la kimataifa.
Profesa Nombo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za elimu na sekta binafsi katika kuwaandaa vijana wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na ushindani wa kimataifa.
Amesema mashindano hayo yamewakutanisha wanafunzi kutoka taasisi mbalimbali, zikiwemo vyuo vya ufundi na teknolojia pamoja na taasisi za sekta binafsi, kwa lengo la kuiwakilisha Tanzania kwa pamoja bila kujali kama taasisi ni ya Serikali au binafsi.
Aidha, Profesa Nombo amesema Serikali imezingatia dhana ya elimu jumuishi katika mashindano hayo kwa kuwapa nafasi vijana wenye mahitaji maalumu kushiriki na kuonesha uwezo wao.
Amesema ushiriki wa vijana hao unathibitisha kuwa changamoto za ulemavu si kikwazo cha mtu kushiriki katika maendeleo ya taifa, akisisitiza kuwa vijana wote wanapaswa kupewa fursa sawa ya kutumia vipaji na ujuzi wao.
“Ulemavu si kutokuwa na uwezo. Hapa tumeona vijana wenye mahitaji maalumu wakifanikiwa kutoka ngazi za chini hadi kufikia hatua hii na kuonesha uwezo wao,” amesema.
Profesa Nombo amesema Wizara itaendelea kuratibu mashindano hayo pamoja na wadau mbalimbali ili kuhakikisha Tanzania inapata vijana wenye ujuzi wa kiwango cha juu watakaoweza kushindana na kufanya vizuri katika mashindano ya Afrika na kimataifa.

More Stories
Kampuni ya Algeria kuwekeza viwanda vya korosho Tanzania
Teknolojia yaibua fursa mpya kwa wanafunzi Wasioona
Diplomasia ya Uchumi Kuimarisha Nafasi Tanzania Kiuchumi