December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yatoa msaada kwa shule nne wilayani Mufindi

Na MwandishiWetu, TimesMajira Online, Mufindi

BENKI ya NMB imetoa misaada ya vifaa mbalimbali vyenye thamani zaidi ya shilingi milioni 17.3 kusaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii katika Wilayani Mufindi.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na madawati 50 kwa ajili ya shule ya Msingi Upendo, Viti 12 na meza 12 kwa shule ya Isupilo na Mabati 200 kwa shule za msingi Nyamalala na Amani yenye lengo la kuezekea madarasa.

Akizungumza mara baada ya kupokea misaada hiyo, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Joseph Mchina, ameishukuru NMB kwa kuendelea kuchangia shughuli za maendeleo wilayani humo.

“Misaada hii imekuja wakati muafaka kwani itasaidia sana kupunguza uhaba wa madawati kwa shule zetu na pia kukamilisha baadhi ya madarasa ambayo yalikuwa yameshajengwa lakini nguvu zilikuwa zinahitajika katika kuezeka, nawashukuru sana NMB,” amesema Mchina.

“Benki ya NMB imekuwa maili kwenye kuunga mkono juhudi za maendeleo za wananchi na kuisaidia Serikali kuboresha huduma za jamii. Naguswa na jinsi mnavyoendelea kutushika mkono sisi watu wa Mufindi na tunaomba msichoke kutusaidia,” ameongeza.

Aidha Mchina amesema, ifike wakati wananchi waone umuhimu wa benki ya NMB katika kujitoa kwao na zawadi pekee ni kuwaunga mkono katika kufungua akaunti na kutumia benki hiyo kuweza kupata faida zaidi ili nao watoe zaidi kwa jamii katika sekta mbalimbali.

Naye Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Straton Chilongola ameushukuru uongozi wa wilaya kwa juhudi zake za maendeleo ya wananchi kwani ni wadau wakubwa kwa mafanikio ya benki hiyo.

Amesema, NMB inatambua mchango wa serikali kwenye kusaidia na kuweka mazingira wezeshi ya biashara wilayani Mufindi kwa mantiki hiyo nayo itaendelea kuwekeza kwa namna mbalimba ili kuwawezesha wananchi ambao ndio wadau wakubwa.

Akizungumzia changamoto za sekta ya elimu na afya kwa NMB ni jambo la kipaumbele linalo hitaji kuunganisha nguvu kulikabiri.

“Ingawa Serikali inafanya makubwa, sisi kama wadau tuna wajibu wa kuunga mkono juhudi hizi za maendeleo kwa kusaidia jamii kwani kupitia jamii hii, ndio imeifanya Benki ya NMB kuwa hapa ilipo na kubwa kuliko benki yoyote hapa nchini.

“Sisi kama NMB tumekuwa mstari wa mbele kuchangia huduma za jamii kwa lengo la kurejesha sehemu ya faida yetu. Kwa zaidi ya miaka 10 mfululizo tumekuwa tukichangia asilimia moja ya faida yetu kila mwaka kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayo tuzunguka,”amesmema Chilongola.

Nao wanafunzi wa shule zilizosaidiwa walisema, msaada waliopata ni motisha tosha ya wao kufanya vizuri kitaaluma na Walimu wakuu pia wamesema mchango wa NMB si tu nisehemu ya kurudisha fadhira kwa jamii lakini pia ni mchango mkubwa katika juhudi za kuboresha elimu nchini.

Chilongola ameongeza kuwa NMB inatambua juhudi za serikali kusimamia elimu na afya kwa nguvu zote kwa kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari na kuboresha huduma za elimu na afya mjini na vijijini, hivyo kama wadau kuna wajibu wa kuunga mkono juhudi hizo za maendeleo kwa jamii kwani ndio wameifanya benki ya NMB kuwa ilipo na kuwa benki kubwa kuliko zote nchini

Meneja wa NMB Mafinga, Mary Mpasha amesema ushirikiano unaotolewa unasababisha biashara ya benko hiyo kukua zaidi na kuifanya kutoa faida kwa jamii inayowazunguka kama benki bora nchini kwa sasa na yenye matawi mengi zaidi.