Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Timu ya riadha ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki – Nje Jogging imeshiriki mashindano ya Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro (Kilimanjaro International Marathon 2024) na kujinyakulia medali 20 leo Februari 25, 2024 Moshi, Kilimanjaro.
Timu hiyo yenye jumla ya wanariadha 30 imeongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Balozi Said Shaibu Mussa.
Katika mbio hizo, wanariadha 10 wameshiriki mbio za Kilometa tano (05) – (Fun run) na wengine 20 wameshiriki mbio za umbali wa kilometa 21 (Tigo half Marathon) ambazo pia Balozi Shelukindo alishiriki.
Akizungumza mara baaada ya kushiriki mbio hizo, Balozi Shelukindo amesema Wizara imeshiriki ili kuunga mkono Kili Marathon ambayo ni moja ya jukwaa la kuutangaza Mlima Kilimanjaro na Tanzania, lakini pia kutangaza majukumu ya Wizara katika mbio hizo. Kadhalika, Dkt. Shelukindo amewasihi waandaaji wa Kili Marathon kwa wakati ujao kuhakikisha kuwa wanashirikiana na Balozi za Tanzania Nje ya nchi ili kuitangaza Kili Marathon zaidi Duniani na kuifanya kuwa bora zaidi ya sasa.
“……………Kilimanjaro ni moja kati ya vivutio vya urithi wa dunia, hivyo kupitia mashindano ya mbio za Kilimanjaro International Marathon tutaweza kutangaza zaidi Kilimanjaro duniani,” alisema Dkt. Shelukindo.
“Tumefurahi kwa kweli kwa kuwa mbio hizi zimefanyika katika mazingira salama, hivyo natoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira salama hapa nchini ambayo yamewawezesha washiriki kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni kushiriki.
Kadhalika, Balozi Shelukindo amewaasa vijana hususan watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na majukumu waliyonayo wajikite katika kufanya mazoezi kwa wingi na nidhamu ili kuwawezesha kushiriki kwa wingi katika michezo ya aina hiyo na mingine na kushinda medali mbalimbali.
Mgeni rasmi katika mbio hizo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro amewapongeza waandaaji wa mbio hizo ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha michezo nchini pamoja na kuibua vipaji vipya vya riadha kwa kila mwaka.
“Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na waandaaji wa mbio hizi, pamoja na wadhamini wakuu na wadau wengine wa michezo katika kuhakikisha mbio hizi zilizoanzishwa zaidi ya miaka 20 iliyopita zinakuwa endelevu kwa manufaa ya maendeleo ya michezo nchini”, amesema.
Katika mbio hizo, Augustino Sulle (Tanzania) ameshinda kilomita 42 kwa wanaume akitumia saa 02:21:06, mbele ya Abraham Kosgei (Kenya) ambaye alitumia saa 02:22:02. Kwa upande wa wanawake, Natalia Sulle (Tanzania) alikuwa mshindi wa kwanza ambapo alitumia Saa 02:51:23, akimtangulia Mtanzania mwenzake Neema Sanka aliyetumia saa 02:51:47, akifuatiwa na Vailet Kidasi katika nafasi ya tatu baada ya kukimbia kwa saa 03:01:03 na hivyo kukamilisha ushindi wa Watanzania kwa nafasi zote tatu za kwanza kwa umbali wa kilomita 42.
Kwa upande wa wanaume mbio za Tigo Half Marathon, Faraj Damas (Tanzania) aliibuka mshindi baada ya kutumia saa 01:16:40, akifuatiwa na Peter Mwangi (Kenya) aliyetumia saa 01:23:44, huku Mtanzania Kennedy Abel akishika nafasi ya tatu baada ya kukimbia mbio hizo kwa muda wa saa 01:24:22.
Kwa upande wa wanawake, wariadha wa Tanzania walitawala mbio hizo za Tigo Half Marathon ambapo Failuna Matanga (Tanzania) aliibuka mshindi baada ya kutumia saa 01:16:40 akifuatiwa na Neema Kisuda (Tanzania) katika nafasi ya pili baada ya kukimbia kwa saa 01:16:54, na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Neema Mbua (Tanzania) baada ya kukimbia kwa saa 01:17:07.
Mbio za mwaka huu zimeshirikisha zaidi ya mataifa 56 na idadi ya wanariadha ikiwa ni zaidi ya 10,000 kutoka ndani na nje ya nchi walishiriki katika mbio hizo. Aidha, mbio hizo zilijumuisha mbio za Kilimanjaro premium lager 42km, 21km Tigo Half marathon na Gee Soseji 5km fun run. Mbio hizo zimeongeza umaarufu wa mbio hizo, katika ukanda wa Afrika Mashariki.
More Stories
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship
Mnzava apania kuwapeleka vijana Simba na Yanga