December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Profesa Zacharia Mganilwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea handaki (njia ya treni) lililopo eneo la Mkadage wilayani Kilosa mkoani Morogoro ikiwa ni ziara ya kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).

NIT yaahidi kuzalisha wataalamu wa kutosha

Na Grace Gurisha,TimesMajira,Online

MKUU wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Profesa Zacharia Mganilwa amesema wamefanya ziara katika Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa lengo la kuangalia changamoto ya rasilimali watu katika miradi mikubwa ya Serikali na kubaini kuwa Tanzania bado inakabiliwa na upungufu wa wataalamu wa masuala ya Reli.

Profesa Mganilwa amesema hayo jana wakati wa ziara ya Baraza la Uongozi wa chuo hicho, ambao walitembelea Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na kuweza kuona handaki la kupita treni ya umeme (treni ya kisasa) na kuona namna ya  ujenzi wa reli unavyoendelea.

Mkuu huyo amesema handaki hilo lina urefu wa Kilomita 1.003 sawa na Mita 1131 ambalo lipo eneo la Mkadage Wilayani Kilosa mkoani Morogoro, ambapo itakuwa imeondoa tatizo la reli kusombwa na maji ya mto Mkondoa.

Amesema hivi sasa, chuo kinaelekeza nguvu zake katika kuzalisha wataalamu ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano ambayo imejielekeza katika uchumi wa viwanda jambo ambalo limetiliwa mkazo na chuo kwa kuzalisha wataalamu hao wa sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya reli.

Profesa Mganilwa amesema wataalamu wakiwepo kwa wingi hasa katika sekta muhimu za uzalishaji na Usafirishaji ndiyo maana wanataka kuzalisha wataalam wa masuala reli nchini kwa lengo la kuokoa fedha za kuwasomesha wengine nje ya nchi.

“Zitakapotangazwa kazi za wakandarasi wa kitanzania wataweza kushindana na wale wa nje na itafikia wakati tunaweza tusiwe na wakandarasi kutoka nje kuja kuchukua miradi mikubwa ya hapa nchini, chuo kinajitaidi kuandaa mitaala mipya kwa lengo la kuongeza wataalam,” amesema Profesa Mganilwa

Aidha, amesema NIT kwa kushirikiana na Serikali kitahakikisha nchi inapata wataalamu wengi wazawa ambao kwa miaka ijayo wao ndio watakaojenga reli za kisasa na madaraja makubwa hapa nchini bila kutegemea nguvu kutoka nje.

“Tanzania tayari imeshafikia katika uchumi wa kati hivyo ni muhimu kuwepo kwa wataalamu wa kutosha ambao wataweza kujenga miundombinu ya reli ya kisasa na barabara kwa lengo la kuendelea kuinua uchumi wa nchi,” amesema

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa amelishukuru Baraza la NIT kwa kutembelea shirika hilo na kuongeza kuwa wataalamu wengi upande wa usafirishaji waliopo TRC wametokea katika chuo hicho.

Amesema NIT ni chuo muhimu katika Shirika lao kwani zaidi ya trlioni saba zimewezwa katika mradi wa SGR na ili kuwa na reli imara lazima wapatikane wataalamu wa kutosha wa kusimamia sekta hiyo.

Mkurugenzi huyo, amesema ili wapatikane wataalamu hao lazima, chuo kiwepo kwa sababu hata kazi za utafiti zifanywe na chuo sio taasisi na pia hata za mafunzo yanatakiwa yatolewe chuo , kwa hiyo ziara hiyo italeta mapinduzi makubwa.

Meneja Msaidizi wa SGR kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro,  Ayoub Mdachi amesema kwa sasa ujenzi wa SGR kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro umefikia asilimia 87 lakini kipande cha Morogoro hadi Makotopola umefikia asilimia 35.

Mtaalamu na Msimamizi wa ujenzi  wa mahandaki ya reli katika mradi wa SGR, Amiry Hamis amesema katika mradi huo kuna  mahandaki manne yenye  urefu wa mita 2620.

“Hivi sasa maendeleo ya mahandaki haya ni mazuri kwani yote yameshamalizika kuchimbwa na kazi iliyobaki ni kuyajengea zege juu ambapo handaki la pili limeshakamilika kwa asilimia 100, ” amesema Hamis