March 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dkt. Wilson Charles

NEC yavionya vikali vyama vinavyotukana

Esther Clavery,TUDARCo na Irene Clemence

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema itaanza kuvichukulia hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kuvifungia kufanya kampeni vyama vya siasa ambavyo wagombea wake watabainika kutumia lugha ya matusi kwenye kampeni.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurungezi wa Uchaguzi wa NEC, Dkt, Wilson Charles, wakati akifungua mkutano kati ya Tume hiyo na watoa huduma ya habari ya mtandaoni .

“NEC inavionya vyama vya siasa vinavyofanya kampeni kwa kutumia lugha za matusi kuacha mara moja na vitakavyobainika vitachukuliwa hatua kali za kisheria,”alisema Dkt. Charles.

Alisema wamefikia uamuzi huo baada ya baadhi ya vyama vya siasa kuendesha kampeni zake kwa kutumia lugha ya matusi badala ya kunadi sera. Alisema vyama hivyo vimekuwa vikitumia maneno ya kashfa, kejeli, udhalilishaji pamoja na vitisho.

Alisema lugha ambazo wamekuwa wakizitoa zinaweza kuchochea uvunjifu wa amani au kuashiria ubaguzi wa jinsia, ulemavu, rangi au maumbile kwenye mikutano na kwenye shughuli zote za kampeni.

“Kuazia sasa tutachukua hatua kwa chama chochote kinachotoa matamko makali katika kampeni badala ya kunadi sera, hatua kali za kisheria zinafanya kazi, hivyo kwa atakeyabainika tutamfungia kuendelea kufanya kampeni,”alisema Dkt. Mahera.

Alisema katika kipindi hiki cha uchaguzi sheria zilizowekwa zitaendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria. Akitolea mfano, alisema hivi karibuni kuna mgombea alikuwa katika jimbo fulani jijini Dar es Salaam ambapo alitumia lugha maneno ya kumkashifu mwezake, jambo ambalo ni kinyume na sheria za uchaguzi.

Alisema kampeni za uchaguzi zinasimamiwa na maadili ya uchaguzi, hivyo Tume kwa kushirikiana na vyama vya siasa na Serikali.

Pia aliongeza kuwa NEC haitafanya kazi kwa mashinikizo ya mataifa ya nje, hivyo vyama hivyo vinapaswa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

***Bajeti ya uchaguzi

Dkt. Charles alisema katika kuandaa na kuendesha uchaguzi mkuu mwaka huu, Tume hiyo iliandaa bajeti ya kiasi cha sh. 331,728,258,035.00 ambazo zinatarajiwa kutumika.

“Kwa kuzingatia kifungu cha 122 cha sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mfuko mkuu wa hazina itagharamia shughuli zote za uchaguzi kwa asilimia 100,”alisema.

***Vifaa

Alisema NEC inaendelea na mchakato wa ununuzi wa vifaa mbalimbali, sambamba na uchapishaji wa fomu, sheria za uchaguzi, kanuni na maelekezo.

Dkt Mahera alisema jumla ya zabuni 25 zimetangazwa ambazo zinahusisha uchapishaji wa nyaraka mbalimbali za uchaguzi na ununuzi wa vifaa.

Kuhusu mapingamizi

Akitolea ufanunuzi kuhusu zoezi la kusikiliza na kutoa rufaa za wagombea, alisema zoezi hilo linatarajiwa kukamilika leo, hivyo Tume hiyo itajikita katika kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi

“Kwa sasa Tume ipo katika zoezi la kusikiliza na kutoa uamuzi wa rufaa mbalimbali ambapo tunatarajia kukamilisha zoezi hili siku ya leo,”alisema .

***Wito

Aidha aliwataka watoa huduma mtandaoni kutokuchoka na kuwasisitiza wadau na wananchi kwa ujumla kuzingatia sheria za uchaguzi, kanuni na maelekezo ya Tume.

Alisema NEC nayo itaendelea kuzingatia sheria za uchaguzi na kanuni zilizotungwa chini yake katika michakato ya uchaguzi kwa kuzingatia katiba,sheria,kanuni na taratibu mbalimbali sinazosimamia uendeshaji wa uchaguzi.